22 Agosti 2020 - 10:16
Ismail Haniya: Makubaliano ya Imarati na Israel ni ‘kulipiga jambia kwa nyuma’ taifa la Palestina

Mkuu wa Idara ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amekosoa vikali makubaliano ya Imarati na utawala haramu wa Israel ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na kusisitiza kwamba, ndoto za alinacha ndizo zilizoufanya utawala wa Abu Dhabi kuchukua hatua kama hiyo, lakini kutaandaliwa mkakati wa kitaifa kwa ajili ya kukabiliana na hatua hiyo.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Ismail Haniya amesisitiza kuwa, taifa la Palestina katu halitasalimu amri na kwamba historia haitawasamehe watu ambao wameanzisha uhusiano wa kawaida na utawala vamizi wa Israel.

Kiongozi huyo wa HAMAS ameongeza kuwa makubaliano ya Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na utawala ghasibu wa Israel ni kulipiga taifa la Plaestina kwa nyuma kwa kutumia jambia na huko ni kukiuka wazi harakati ya kihistoria, Kiarabu na Kiislamu kuhusiana na kadhia ya Palestina.

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina amewataka Waislamu na wapigania haki kote ulimwenguni kusimama kukabiliana na hatua za kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala vamizi wa Israel.

Kufuatia hatua kadhaa zilizochukuliwa na Rais Donald Trump wa Marekani kwa lengo la kurahisisha uanzishwaji wa uhusiano wa kawaida kati ya Imarati na utawala haramu wa Kizayuni, Alkhamisi iliyopita ya tarehe 13 Agosti pande mbili za Abu Dhabi na Tel Aviv zilisaini mkataba na kuafikiana rasmi kuanzisha uhusiano kamili wa kidiplomasia.

Makubaliano hayo kati ya Israel na Imarati yamekabiliwa na wimbi kali la malalamiko na upinzani wa makundi ya Palestina, nchi za Kiislamu katika eneo la Asia Magharibi na shakhsia kadhaa wa kisiasa duniani, ambao karibu wote wamesisitiza kwa kauli moja kuwa, hatua hiyo ya Imarati ni uhaini na usaliti kwa malengo matukufu ya Palestina.

342/