Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Baada ya serikali ya Ankara kuuhujumu kwa maneno makali Umoja wa Ulaya, Mkuu wa Siasa za Nje wa umoja huo Josep Borrell ameituhumu Uturuki kuwa inataka kuhuisha utawala wa Ottoman Empire. Borrell ameashiria harakati za hivi karibuni za Uturuki katika eneo la mashariki mwa Bahari ya Mediterania na kusema kuwa, kuiwekea vikwazo Ankara ni miongoni mwa njia zenye taathira kubwa katika kukabiliana na chokochoko za Uturuki.
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian pia amesema kuwa, suala la kuiwekea vikwazo Uturuki litajadiliwa katika kikako kijacho cha Bunge la Ulaya na kuna uwezekano wa kuchukuliwa hatua kamili dhidi ya Ankara. Awali viongozi wa Ugiriki pia walikuwa wamewataka wenzao wa Umoja wa Ulaya kuiwekea vikwazo Uturuki kwa sababu ya kukika mipaka ya baharini huko mashariki mwa Bahari ya Mediterania.
Katika miezi ya karibuni Uturuki imezidisha operesheni za kusaka mafuta na gesi katika Bahari ya Aegean mashariki mwa Mediterania, suala ambalo limezikasirisha mno nchi jirani za kusini magharibi mwa nchi hiyo hususan Ugiriki na Cyprus. Ankara inadai kuwa, kufuatia kusambaratika utawala wa Kiothmani (Ottoman Empire) baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia na makubaliano ya baada yake, Uturuki iliondolewa katika maeneo mengi na visiwa vilivyoko katika Bahari ya Aegean na mashariki mwa Bahari ya Mediterania. Hivi karibuni Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki alisema kuwa: Ankara haikubali kuendelea kuzuiliwa katika maeneo ya pwani.
Kwa msingi huo katika miezi ya karibuni Ankara ilianzisha operesheni za kusaka gesi na mafuta karibu na kandokando ya visiwa vya Ugiriki na jambo hilo limeifanya iwajihiane uso kwa uso na Athens na Umoja wa Ulaya. Ugiriki inasema maeneo hayo ni milki yake. Hali hii imezusha mgogoro na mivutano baina ya pande hizo mbili.
Kuongozeka mivutano baina ya Uturuki na baadhi ya wanachama wa Umoja wa Ulaya juu ya maliasi ya gesi na mafuta huko mashariki mwa Bahari ya Mediterania kunaifanya Ankara iwe mbali zaidi na Umoja wa Ulaya na kuzidisha malumbano baina ya pande mbili. Joseph Hincks ambaye ni mtaalamu wa masuala ya siasa wa Marekani anasema: Umoja wa Ulaya umesimama kidete kuiunga mkono Ugiriki na umeitahadharisha Ankara kuhusu operesheni yake ya kusaka gesi na mafuta katika maeneo na baharini.
Inaonekana kuwa miongoni mwa malengo ya Ankara katika operesheni hiyo ni kutaka kutazamwa upya hali ya kisheria ya visiwa vya Ugiriki vilivyoko karibu na pwani ya Uturuki na kuulaimisha Umoja wa Ulaya kuunga mkono matakwa ya Uturuki. Hata hivyo jambo hili linaonekana kuwa gumu na huwenda muhali kwa kutilia maanani msimamo wa Umoja wa Ulaya wa kuziunga mkono kikamilifu Ugiriki na Cyprus. Si hayo tu, bali baadhi ya nchi za Ulaya tayari zimechukua hatua za kivitendo za kuiunga mkono Ugiriki mkabala wa Uturuki. Kwa mfano tu Ufaransa imechukua hatua ya kuiuzia Ugiriki ndege 10 za kisasa za kijeshi za Rafale na kuipa bure ndege nyingine 8. Ufaransa pia imetuma kikosi cha majeshi yake ya majini katika eneo linalozozaniwa.
Uhusiano wa Uturuki na Umoja wa Ulaya umekuwa na mivutano mingi tangu baada ya jaribio lililoshindwa la mapinduzi nchini Uturuki mwezi Julai mwaka 2016. Jaribio hilo lilipelekea kusitishwa mchakato wa kujiunga Uturuki katika umoja huo. Wakati huo huo Brussels imekuwa ikikosoa sana siasa za ndani za Uturuki na suala la kubadilishwa muundo wa kisiasa wa nchi hiyo kutoka mfumo wa Bunge na kuwa wa Rais wa Jamhuri. Katika miaka miwili ya karibuni pia hitilafu kali za pande hizo kuhusu hatua ya serikali ya Ankara ya kutuma majeshi yake huko kaskazini mwa Syria na vilevile kuingilia vita vya ndani nchini Libya, zimezidisha sana ufa na mivutano baiya ya EU na Uturuki.
Umoja wa Ulaya unapinga vikali hatua ya Uturuki ya kusaka mafuta na gesi katika maeneo ya kandokando ya Ugiriki na Cyprus na katika kadhia hiyo umeegemea kikalimifu upande wa wanachama hao wawili wa EU. Brussels inasema operesheni hiyo ya Uturki inakiuka sheria na imeitahadharisha Ankara kwamba iwapo haitasitisha operesheni hiyo itakabiliwa na "jibu linalofaa".
Inavyoonekana ni kuwa kwa sasa Umoja wa Ulaya umeamua kuiwekea Uturuki vikwao vya kiuchumi. Ankara kwa upande wake inasisitiza kuwa, itajibu ngumi moja kwa makonde mawili. Sambamba na hayo Brussels imesisitiza udharura wa kufanyika mazungumzo kwa ajili ya kuupatia ufumbuzi mgogoro huo .
342/