2 Novemba 2020 - 12:53
Sisitizo la Rais mteule wa Bolivia la kuunga mkono kadhia ya Palestina

Baada ya chama cha mrengo wa kushoto nchini Bolivia kuibuka mshindi katika uchaguzi wa Rais nchini humo, Luis Arce rais mteule wa nchi hiyo amesisitiza juu ya himaya na uungaji mkono wa nchi yake kwa kadhia ya Palestina katika majukwaa na duru zote za ndani na za kimataifa.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Akizungumza na balozi wa Palestina nchni Bolivia, Rais mteule Luis Arce ambaye anatarajiwa kuapishwa Novemba 8 mwezi huu amesisitiza kuwa, nchi yake itatumia duru zote za ndani na za kimataifa kuiunga mkono kadhia ya Palestina na kwamba, serikali ya La Paz itashirikiana na Palestina katika katika nyanja zote. 

Uchaguzi wa Rais nchini Bolivia ulifanyika tarehe 18 ya mwezi uliopita wa Oktoba ambapo Luis Arce mgombea wa chama cha Movement For Socialism "Harakati Kwa Ajili ya Ujamaa' ambaye ni mtu wa karibu wa Evo Morales Rais wa zamani wa nchi hiyo aliibuka mshindi baada ya kujikusanyia asilimia 52 ya kura.

Morales na chama chake kwa miaka mingi wamekuwa wakiunga mkono malengo matukufu ya Palestina na wakati huo huo kukosoa vikali siasa za kidhalimu za utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Wapalestina.

Ukweli wa mambo ni kuwa, siasa zilizo dhidi ya ukoloni na dhidi ya ubepari za viongozi wa mrengo wa kushoto wa Amerika ya Latini akiwemo Evo Morales, zimepelekea nchi za mrengo wa kushoto za eneo hilo daima zikabiliwe na mashinikizo ya wazi na ya siri ya Marekani, kiasi kwamba, wanajeshi nchini Bolivia wakiungwa mkono na Marekani walifanya mapinduzi baridi na kumuondoa madarakani Morales. Kwa miezi kadhaa sasa Jeanine Anez Chavez anashikilia uongozi wa nchi kama Rais wa muda ambapo anaendesha siasa za uhafidhina na kufurutu ada.

342/