2 Februari 2021 - 12:47
Msemaji wa Taliban: Iran inatoa mchango chanya katika mazungumzo ya amani ya Afghanistan

Msemaji wa ofisi ya kisiasa ya Taliban mjini Doha, Qatar amesema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatoa mchango chanya na athirifu katika mchakato wa mazungumzo ya amani ya Afghanistan.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Suhail Shaheen ameyasema hayo katika mahojiano na shirika la habari la Iran Press, ambapo sambamba na kuashiria kuwa Iran na Afghanistan ni nchi mbili jirani hivyo inapasa ziwe na ushirikiano wa kudumu; amesisitiza kwamba kundi la Taliban linapinga uvamizi wa Marekani na kuikalia kwa mabavu Afghanistan.

Msemaji wa ofisi ya kisiasa ya Taliban mjini Doha amebainisha kuwa, Marekani iliivamia na kuikalia kwa mabavu Afghanistan yapata miaka 20 iliyopita na kwa sababu hiyo kundi la Taliban limesimama kukabiliana nayo na kupambana na nchi hiyo kwa kuikalia kwa mabavu ardhi ya Afghanistan.

Suhail Shaheen ameeleza pia kwamba, lengo la mazungumzo ya amani ya Afghanistan ni kutatua masuala ya nchi hiyo na kwamba makundi yote ya jihadi yanahudhuria mazungumzo hayo na kujadili kwa pamoja matatizo ya nchi yao.

Baada ya ziara yake ya siku kadhaa hapa nchini ya kushauriana na kufanya mazungumzo na maafisa waandamizi wa Iran akiwemo waziri wa mambo ya nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mohammad Javad Zarif, ujumbe wa kisiasa wa Taliban jana ulifanya mkutano na vyombo vya habari hapa mjini Tehran na kujibu masuali mbalimbali ya waandishi wa habari.../

342/