19 Machi 2021 - 17:46
White House: Biden hajutii matamshi yake dhidi ya Rais wa Russia

Msemaji wa Ikulu ya Marekani, White House amesema kuwa, rais wa nchi hiyo, Joe Biden hajutii matamshi yake aliyoyatoa dhidi ya rais mwenzake wa Russia, Vladimir Putin. Katika mahojiano ya televisheni, Biden alimwita Putin kuwa ni muuaji.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Msemaji wa White House, Jen Psaki, jana Alkhamisi aliwaambia wanaandishi wa habari kuwa, Rais wa Marekani hajutii hatua yake ya kumwita Putin kuwa ni muuaji. 

Baada ya matamshi hayo, Rais Vladimir Putin wa Russia alikanusha madai ya Joe Biden na kusema, namuombea kila la kheri Biden; inashangaza kumuona muuaji akiwaita wengine kuwa ni wauaji.

Baada ya hapo, Naibu Mkuu wa Baraza la Shirikisho (Bunge la Seneti la Russia) alisema kuwa, Marekani inapaswa kuomba radhi kwa hatua yake ya kumtukana Rais Vladimir Putin wa Russia.

Konstantin Kosachev jana Alkhamisi aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: hatua ya kumuita Moscow Anatoly Antonov Balozi wa Russia mjini Washington ni jibu sahihi kwa matamshi ya Rais Joe Biden wa Marekani. 

Kosachev ameongeza kuwa, matamshi kama hayo hayakubaliki kivyovyote vile; na yanavuruga zaidi uhusiano wa pande mbili. Naibu Mkuu wa Baraza la Shirikisho (Bunge la Seneti la Russia) amebainisha kuwa, kitendo cha kumuita nyumbani Balozi wa Russia mjini Washington haitakuwa radiamali ya mwisho ya Kremlin kwa matamshi ya Biden iwapo Marekani haitaomba radhi.

Mara chungu nzima Russia imekuwa ikikanusha kujihusisha kivyovyote vile na masuala ya ndani ya Marekani ikiwemo uchaguzi wa nchi hiyo.

342/