24 Aprili 2021 - 10:51
Kwa mara nyingine Rais wa Ufaransa atoa maneno ya chuki dhidi ya Uislamu

Kwa mara nyingine tena, rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron ametoa maneno ya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa kutumia kisingizio cha kushambuliwa polisi mmoja mwanamke kwa silaha baridi.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Usiku wa kuamkia leo Jumamosi, kwa mara nyingine rais wa Ufaransa ameuhusisha Uislamu na vitendo vya kigaidi na kuandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: "Hatutorudi nyuma katika kupambana na 'ugaidi' wa Kiislamu."

Jana jioni, polisi mmoja mwanamke alishambuliwa kwa silaha baridi katika viunga vya mji mkuu wa Ufaransa, Paris na shambulio hilo limetumiwa na Macron kuonesha chuki zake zisizo na kikomo dhidi ya dini tukufu ya Kiislamu. Tukio hilo lilitokea katika lango la kuingilia jengo la idara ya polisi mjini Rambouillet, nje ya mji wa Paris.

Polisi wa Ufaransa wanadai kuwa mshambuliaji alikuwa na asili ya Tunisia na ameuawa kutokana na majeraha aliyopata wakati wa kutiwa mbaroni.

Vyombo vya habari vya Ufaransa ambavyo navyo vinafuata misimamo ya chuki dhidi ya Waislamu na Uislamu kama ilivyo misimamo ya serikali ya nchi hiyo, vimedai kuwa, sauti ya Allahu Akbar ilisikika wakati polisi huyo aliposhambuliwa kwa kisu, hivyo Waislamu ndio waliofanya shambulio hilo kwa mtazamo wa vyombo hivyo vya habari vya Ufaransa.

Kabla ya hapo, wabunge wa Ufaransa walikuwa wamepasisha sheria ya kuwapiga vita waziwazi Waislamu na dini yao tukufu.

Sheria hiyo ina vifungu 70 na inairuhusu serikali ya Ufaransa kufunga skuli zote za Wasialmu na maeneo yao ya ibada na vile vile kupiga marufuku khutba na mawaidha wakati wowote inapohisi hayaendani na utamaduni wa Kimagharibi na wa kisekula wa Ufaransa.

342/