19 Mei 2021 - 13:03
Sisitizo la Rouhani la kulindwa usalama wa kiafya wa wananchi kwa ajili ya kuongeza ushiriki wao katika uchaguzi

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza udharura wa kulindwa usalama wa kiafya wa wananchi ili kuwahamasisha washiriki kwa wingi katika uchaguzi mkuu ujao wa rais.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Akizungumza jana Jumanne katika kikao cha wakuu wa kamati za kitaalamu za tume ya kupambana na maradhi ya corona, Rais Rouhani amesema kudhiminiwa usalama wa kiafya wa wananchi kuna nafasi muhimu katika kuwashajiisha washiriki kwa wingi katika uchaguzi.

Rais Rouhani amesema, wananchi wanapasa kupata imani kwamba usalama wao wa kiafya unadhaminiwa katika hatua zote za kampeni za uchaguzi na wakati wa kufanyika uchaguzi wenyewe.

Amewataka wasimamizi wa masuala yote yanayohusiana na uchaguzi mkuu huo wahakikishe kwamba usalama wa roho na afya za wananchi unapewa kipaumbele katika hatua zote za uchaguzi. Amesisitiza kwamba hatua zote zinazotishia na kuhatarisha usalama wa raia zinapaswa kuepukwa.

Rais wa Iran amesesisitiza kufuatwa na kutekelezwa kwa makini maelekezo na miongozo yote ya Wizara ya Afya kwa ajili ya kukabiliana na janga la corona.

Duru ya 13 ya uchaguzi wa rais wa Iran imepangwa kufanyika tarehe 28 mwezi ujao wa Khordad, sawa na Ijumaa tarehe 18 Juni.

342/