ABNA24 : Sayyid Asadollah Avaei ambaye mapema leo alikuwa akizungumza na Shirika la Habari la Iran, IRNA kwa mnasaba wa kumbukumbu ya siku ya kuaga dunia Imam Ruhullah Khomeini amesema, katika upande wa kisiasa hayati Imam Khomeini alikuwa mweledi, mtu mwenye maono ya mbali na hodari sana. Ameongeza kuwa, Imam Khomeini alianza kufuatilia masuala ya kisiasa ya dunia tangu alipokuwa kijana na alitabiri suala la kuporomoka mfumo wa ukomunisti wa kambi ya Mashariki na ustaarabu wa kibepari wa Magharibi katika kipindi ambacho hakuna mwanasiasa hata mmoja aliyefikiria hata kidogo sala hilo.
Mkuu wa Kituo cha Kiislamu cha Manchester amesema: Imam Ruhullah hakuwa na nia ya kuuondoa madarakani utawala wa Shah nchini Iran tu, bali lengo lake lilikuwa kubwa na pana zaidi, yaani kuasisi ustaarabu mpya na mpana zaidi wa Kiislamu.
Avaei ameashiria sehemu moja ya matamshi ya Imam Khomeini akisema: "Tumefanikiwa kufika hapa tulipo kwa harakati hii ya Kiislamu na kuyatimulia vumbi madola ya kibeberu. Tangu sasa tunapaswa kutumia harakati hii ya Kiislamu kwa ajili ya ujenzi na ustawi, na sisi sote tupige hatua mbele kuelekea kwenye ustaarabu sahihi wa mafundisho ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake."
Leo Ijumaa tarehe 14 Khordad kwa mwaka wa Hijria Shamsia inasadifiana na kumbukumbu ya mwaka wa 32 tangu Imam Ruhullah Khomeini alipoaga dunia na kurejea kwa Mola wake Karima.
342/