Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake jijini New York, Marekani kwamba, "nalaani vikali mauaji ya Rais Jovenel Moïse. Watekelezaji wa mauaji hayo lazima wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria."
Vyombo mbalimbali vya habari jana vilimnukuu Waziri Mkuu wa Haiti, Claude Joseph akithibitisha kutokea shambulio na mauaji dhidi ya Rais Jovenel Moïse na kusema kuwa limefanywa na makomandoo waliokuwa na silaha kwa kusaidiwa na mamluki kutoka nje ya Haiti.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametuma salamu za rambirambi kwa wananchi na serikali ya Haiti pamoja na familia ya hayati Moïse.
Amesema Umoja wa Mataifa kwa upande wake utaendelea kushikamana na serikali na wananchi wa Haiti.
Rais Jovenel Moïse amekuwa madarakani tangu mwezi Februari mwaka 2017 na aliingia uongozini kufuatia uchaguzi uliotokana na mtangulizi wake Michel Martelly kujiuzulu.
Wakati huo huo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nalo limetoa taarifa likilaani mauaji ya Rais huyo wa Haiti.
Mwezi Februari mwaka huu, Jovenel Moïse ambaye alikuwa mfanyabiashara wa kuuza nje ndizi kabla ya kuwa mwanasiasa, alisema kwamba polisi wamefanikiwa kuzuia njama ya kumuua.
Haiti ni moja ya nchi maskini zaidi duniani. Mbali na mgogoro wake mkubwa wa kiuchumi na miundombuni mibovu, vifo vinavyotokana na vimbunga vikali, mitetemeko ya ardhi na maradhi ya kuambukiza, nchi hiyo inateswa pia na mizozo mikubwa ya kisiasa kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.
342/