Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Andrew Kirkwood, mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Myanmar amesema kuwa, wananchi wa Myanmar wanakumbwa na mgogoro mbaya ambapo hadi mapinduzi ya kijeshi yanatokea nchini humo Februari mwaka huu, umoja huo ulikuwa ukitoa himaya na msaada kwa watu milioni moja.
Taarifa ya mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Myanmar imeeleza kuwa, hivi sasa idadi ya watu wanaohitajia msaada nchini humo imefikia milioni tatu ikiwa imeongezeka mara tatu katika kipindi cha miezi minane iliyopita.
Aidha amebainisha kuwa, suhula za sasa zilizopo haziwezi kukidhi mahitaji ya idadi hiyo ya wanaohitajia misaada ya kibinadamu katika nchi hiyo.
Jeshi la Myanmar lilitwaa madaraka ya nchi Februari Mosi mwaka huu baada ya kumkamata Rais wa nchi, Win Myint na viongozi wengine akiwemo Aung San Suu Kyi, kiongozi wa chama tawala mwenye ushawishi mkubwa, kufuatia siku kadhaa za mivutano nchini humo.
Kisingizio cha jeshi cha kufanya mapinduzi hayo ni madai yake ya kutokea wizi na udanganyifu katika uchaguzi wa Bunge wa Novemba mwaka jana ambapo chama tawala cha National League for Democracy (NLD) kinachoongozwa na Aung San Suu Kyi kiliibuka na ushindi.
Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa, jeshi la Myanmar limefanya mauaji ya umati nchini humo tangu lilipotwaa madaraka ya nchi kwa mtutu wa bunduki.
342/