24 Machi 2022 - 15:54
Ujerumani yapinga askari wa vikosi vya NATO kupelekwa Ukraine

Kansela Olaf Schultz wa Ujerumani amesema Shirika la kijeshi la NATO katu halitapeleka askari Ukraine na wala halitatekeleza marufuku ya ndege kupaa katika anga ya nchi hiyo.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Tangu miezi kadhaa nyuma, Russia imekuwa ikionya juu ya hatua ya NATO kujipanua kuelekea mashariki ya Ulaya; na hata ikatoa mapendekezo kwa Marekani na shirika hilo la kijeshi ya kupatiwa hakikisho la usalama, lakini mapendekezo hayo yalikatiliwa na pande hizo mbili.

Sambamba na maombi ya mtawalia ya Ukraine ya kutaka kujiunga na shirika la kijeshi la NATO na kupokea misaada ya mamilioni ya dola kutoka nchi za Magharibi, tarehe 24 Februari Russia ilianzisha mashambulio ya kijeshi dhidi ya Ukraine kwa amri ya Rais Vladimir Putin wa nchi hiyo.

Akihutubia bunge la Ujerumani Bundestag, Shultz amesema, Ujerumani haitaki asilani yatokee makabiliano ya ana kwa ana baina ya Russia na Nato.

Kansela wa Ujerumani ameendelea kueleza: "tunasikia maombi ya kututaka tutekeleze mpango wa marufuku ya kupaa ndege na kupeleka askari Ukraine; japokuwa ni jambo gumu, lakini hatutasalimu amri kwa matakwa hayo".

"Miaka 80 iliyopita, yaani baada ya Vita vya Dunia, tulijaribu kuepusha makabiliano ya ana kwa ana kati ya muungano wa kiulinzi wa Magharibi NATO na Russia; na ipo haja ya mwenendo huu kuendelezwa," amesema Kansela Olaf Schultz.

Shultz amesisitiza kuwa, Nato katu haitakuwa upande mwingine wa vita vya Ukraine na kwamba, kuna mwafaka juu ya suala hilo baina ya Ujreumani, waitifaki wake wa Ulaya na Marekani.

Kansela wa Ujerumani ametoa kauli hiyo katika hali ambayo, katika mahojiano ya televisheni aliyofanyiwa jana, Naibu wa balozi wa Russia katika Umoja wa Mataifa Dmitry Polyansky alisema: "si hatua sahihi kuitisha Russia na kuingilia masuala yake ya ndani. Kwa hiyo wakati mnakabiliana na dola lenye nguvu za nyuklia, inapasa mufikirie matokeo ya chochote kinachoweza kutokea kutokana na mwenendo wenu huo."

Vita vya Ukraine, sasa hivi vimeshatimiza takriban mwezi mmoja, na hadi sasa nchi 25 zimeipatia nchi hiyo aina mbalimbali ya silaha na zana za kivita. Vita hivyo vinaendelea huku Russia ikisisitiza kuwa haina nia ya kuikalia kwa mabavu ardhi ya Ukraine.../

342/