21 Aprili 2022 - 12:55
Amnesty International: Vitendo vya Israel dhidi ya Palestina ni "uhalifu dhidi ya ubinadamu."

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeitaja Israel kuwa ni utawala wa kibaguzi na kutangaza kuwa, mauaji na mateso yanayofanywa na utawala huo dhidi ya Wapalestina na kuwanyimwa haki zao ni uhalifu na jinai dhidi ya binadamu.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Amnesty International imeandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: "Ubaguzi wa rangi (apartheid) sio jambo lililopita na la kihistoria tu, bali pia ni ukweli na hakika inayowasumbua kila siku mamilioni ya Wapalestina katika maeneo yao yanayokaliwa kwa mabavu na inaendelea hadi hii leo." 

Shirika hilo la kimataifa la kutetea haki za binadamu limesema: "linafuatilia ripoti zote za mauaji ya kiholela, kukamatwa ovyo, kuteswa na kunyongwa kwa watu wengi huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu."

Amnesty International imesisitiza kuwa, utawala wa kibaguzi unayaona maisha ya kundi moja kuwa muhimu zaidi kuliko maisha ya lingine, na kwamba Israel inaendelea kuwa utawala wa kibaguzi kwa kuwaua, kuwatesa na kuwanyima Wapalestina haki zao za kimsingi. "Huu ni uhalifu dhidi ya ubinadamu na lazima ukomeshwe", imesisitiza taarifa ya Amnesty International.

Awali shirika hilo la kimataifa la kutetea haki za binadamu lilikuwa limetangaza kuwa, kupokonywa ardhi, kobomolewa nyumba, kuuawa kinyume cha sheria, kuvuliwa uraia, kufungwa na kuteswa ni sehemu ya mbinu za mfumo wa apartheid unaotumiwa na Tel Aviv dhidi ya Wapalestina.

342/