23 Oktoba 2022 - 18:38
Sheikh Isa Qassem: Viongozi wa dini mbalimbali msiamini madai ya utawala wa Bahrain

Kiongozi wa kidini wa Mapinduzi ya Bahrain amewataka washiriki wa kongamano la viongozi wa dini duniani wasiamini kaulimbiu na madai ya utawala wa kifalme wa nchi hiyo kuhusu watu kuishi kwa amani na masikilizano.

Tarehe 3 na 4 za mwezi ujao wa Novemba Bahrain itakuwa mwenyeji wa kongamano la kimataifa la dini mbalimbali litakalofadhiliwa na mfalme wa nchi hiyo Hamad bin Isa Aal Khalifa.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, Sheikh Isa Qassem, kiongozi wa kidini wa mapinduzi ya Bahrain ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter: Kongamano hili la Bahrain linaendeshwa kwa kaulimbiu ya "Mashariki na Magharibi kwa ajili ya watu kuishi kwa masikilizano" na utawala unaowakandamiza wananchi wake na kufanya upendeleo baina yao.

Sheikh Isa Qassem ameongezea kwa kusema: huu ni ukweli usiofichika kwa washiriki wa kongamano hili.

Mufti wa Al Azhar Sheikh Ahmad Attayib na Papa Francis, Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani watahudhuria kongamano hilo la viongozi wa dini mbalimbali litakalosimamiwa na Baraza la Mazungumzo la Bahrain na kufanyika kwa kaulimbiu ya "Mashariki na Magharibi kwa ajili ya watu kuishi kwa masikilizano".

Shakhsia zaidi ya 200 wakiwemo viongozi wa dini, wanafikra mashuhuri na wadau wa vyombo vya habari wanatarajiwa kushiriki katika kongamano hilo.

Kongamano la viongozi wa dini mbalimbali litafanyika katika hali ambayo, tangu Februari 14, 2011 Bahrain imekuwa uwanja wa mapambano ya amani ya wananchi dhidi ya utawala wa kiimla wa ukoo wa Aal Khalifa. Wananchi hao wanataka uhuru, kutekelezwe uadilifu na kuondolewa ubaguzi pamoj na kuongozwa na serikali iliyochaguliwa na wananchi wenyewe.

Makundi ya kutetea haki za binadamu yametoa taarifa mara kadhaa kulaani ukandamizaji unaofanywa na utawala wa Bahrain dhidi ya wapinzani na kutoa mwito wa kufanyika mageuzi katika mfumo wa kisiasa wa nchi hiyo.../

342/