Tetemeko la kwanza la ardhi la ukubwa wa 7.8 katika kipimo cha Rishta lilitikisa kusini mwa Uturuki na kaskazini mwa Syria Jumatatu asubuhi ya tarehe 6 Februari. Kitovu chake kilikuwa ni katika mji wa Gaziantep wa Uturuki ambapo mamia ya majengo yameporomoka.Masaa machache baadaye kulijiri mtetemeko mwingine wa ardhi uliokuwa na ukubwa 7.6 kwenye kipimo cha rishta.
Makamu wa Rais wa Uturuki Fuat Oktay alitangaza jana kuwa idadi ya waliofariki nchini humo imefika 24,600 huku taarifa zikisema waliothibitishwa kufariki Syria ni 5,189.
Maelfu ya watu bado hawajulikani walipo, wengine 80,000 wamejeruhiwa na zaidi ya majengo 6,400 nchini Uturuki yameharibiwa, kulingana na takwimu za serikali. Idadi ya vifo sasa imezidi kwa mbali ile ya mitetemeko ya ardhi ya 1999 karibu na Istanbul, wakati takriban watu 18,000 walipoteza maisha.
Ingawa idadi kubwa zaidi ya wahanga wa mitetemeko hiyo imerikodiwa nchini Uturuki, lakini indhari zinazidi kutolewa kuhusu idadi ya vifo kaskazini mwa Syria, kutokana na uwezo mdogo, uhaba wa nyenzo, na kuchelewa kuwasili misaada ya kimataifa inayohitajika kwa shughuli za utafutaji na uokoaji wa watu walionasa chini ya vifusi.
Wakati huo huo, akizungumza katika mji wa Adana uliokumbwa na mitetemeko ya ardhi nchini Uturuki, Martin Griffiths alisema anatarajia makumi ya maelfu ya vifo kuthibitishwa. Griffiths, mratibu wa misaada ya dharura wa Umoja wa Mataifa, alisema: "Nadhani ni vigumu kukadiria kwa usahihi idadi ya waliopoteza masiha kwani tunahitaji kuingia chini ya vifusi lakini nina uhakika itaongezeka maradufu au zaidi.
Huku matumaini ya watu waliokwama chini ya mabaki ya Uturuki na Syria yakififia, Griffiths alisema juhudi za uokoaji sasa ziko katika hatua za mwisho. Ameongeza kuwa, "Wanasema saa 72 ni kipindi cha dhahabu (kwa uokoaji)."
342/