15 Februari 2023 - 19:16
Mapinduzi ya Netanyahu dhidi mfumo wa mahakama na uwezekano wa msambaratiko wa ndani

Rais Isaac Herzog wa utawala haramu wa Israel amekiri kuwa, utawala huo unakaribia kusambaratika kisheria na kijamii.

Kiongozi huyo wa utawala ghasibu amezitaka pande na mirengo yote katikk ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel kuweka kando uwendawazimu na badala yake ziwe pamoja.

Rais Isaac Herzog amesema: Sisi filihali tunakaribia kusambaratika kikatiba na kijamii. Mimi ninahisi -sote tuna hisia hii- kwamba, hatuko mbali sana na masafa ya kusambaratika.

Rais huyo wa Rais amewahutubu Wazayuni kwa kusema: Sisi tunakaribia kutumbukia katika vita vya ndani na mlipuko wa pia la baruti umekaribia mno kuliko wakati wowote ule, na hivyo aina yoyote ile ya utumiaji mabavu dhidi ya viongozi wa Kizayyuni na waungaji mkono wao ni mstari mwekundu.

Rais wa Israel ameeleza kwamba: Utawala huo unapitia siku ambazo ni nyeti na muhimu kwa mustakabali wake na maneno ninayoyasema hivi sasa ni machungu na majuma yaliyopita nimefanya kila hima na jitihada ili kufikia mwafaka, hivyo wote wanapaswa kutambua kwamba, kama upande mmoja utapata ushindi na upande mwingine kushindwa, maana yake ni kushindwa utawala wote wa Kizayuni.Isaac Herzog amewasilisha mpango wa maridhiano ili kuiokoa Israel na kile alichokitaja kuwa, "msambaratiko wa katiba na uwezekano wa kutokea utumiaji mabavu kutokana na mageuzi katikka mfumo wa mahakama ambayo yamezusha makelele na mjadala mkubwa na ambayo yanafuatiliwa na serikali ya mrengo wa kulia ya Benjamin Netanyahu. Sehemu nyingine ya hotuba hiyo adimu ya Rais wa utawala ghasibu wa Israel inajumuisha takwa lake kwa Wabunge waitifaki kufanya kila wawezalo kusitisha sheria hiyo katika hatua yake ya awali Bungeni. Pamoja na hayo kamati ya haki na sheria katika Bunge la utawala haramu wa Israel (Knesset) imekaidi na kupuuza mapendekezo ya Rais wa Israel na badala yake imepasisha mapendekezo ambayo ni kwa maslahi ya serikali ya sasa ya Netanyahu. Mpango huo unaupa uwezo serikali ya muungano ya Netanyahu wa kubana mamlaka ya Mahakama Kuu katika nyanja mbili. Kwa upande mmoja ni kuwa, baraza la mawaziri litakuwa na mamlaka kamili ya kuwateuwa majaji ikiwa ni pamoja na Jaji wa Mahakama Makuu ya utawala huo wa Kizayuni. Katika upande wa pili, mpango huo unabana pakubwa uwezo wa Mahakama Kuu wa kufuta sheria na maamuzi ya serikali. Wanaokosoa mpango huo wanaamini kuwa, Netanyahu na baadhi ya mawaziri wake wanafanya kila wawezalo kuudhofisha muundo wa sasa wa mahakama ili kufunga mafaili ya kesi lukuki zinazowakabili. Wapinzani wanasema kuwa, mpango huo utahitimisha uhuru wa idara ya mahakama ya utawala ghasibu wa Israel na kulifanya suala la kuzuia na kupambana na ufisadi kuwa gumu katika ardhi hizo za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Ala kulli haal, majimui ya ushahidi uliopo unaonyesha kuwa, hakuna upande wowote kati ya pande zinazozana hivi sasa huko Israel ambao uko tayari kulegeza kamba na kufumbia macho mitazamo na misimamo yake na umekuwa ukilitazama hilo kama jambo la kufa na kupona kisiasa. Misimamo hiyo na anga inayyotawala hivi sasa huko Israel ndio inayotia nguvu dhana ya uwezekano wa kutokea msambaratiko ndani ya utawala ghasibu wa Israel. 

342/