3 Machi 2023 - 14:01
Kuongezeka malumbano kati ya serikali ya Netanyahu yenye msimamo mikali na jeshi la Kizayuni

Mamia ya maafisa wa kitengo cha kijasusi cha Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel wameonya kwamba hawatahudumu tena jeshini iwapo mpango wa kurekebisha sheria ya mahakama katika utawala huo utaidhinishwa.

Maafisa wa akiba wa kitengo cha "8200" cha jeshi hilo la kizayuni walitangaza katika barua iliyotumwa kwa Waziri wa Vita, Yoav Galant, Mkuu wa Kamandi Kuu ya Jeshi, Herzi Halevi, na Mkuu wa Idara ya Ujasusi wa Kijeshi, Aron Halifa kwamba: Tunashuhudia ishara za kutisha ambazo zinaibua wasiwasi kuhusu kuhatarishwa usalama wa Israeli."

Barua hiyo inaeleza kuwa wasi wasi wa maafisa hao unahusiana na kusambaratika kwa mafungamano ya kijamii, uharibifu wa uchumi, uthabiti na taswira ya utawala wa Kizayuni duniani kutokana na kufutwa msingi wa kugawana madaraka kati ya mihimili mikuu ya dola ambapo uhuru wa mahakama uko hatarini. Maafisa hao wanasema yamkini mabadiliko  yanayofuatiliwa na serikali ya Netanyahu yakaibua hasara ambazo itakuwa vigumu kuzifidia haraka.

Kadiri muda unavyosonga mbele, pengo kati ya viongozi mbalimbali wa utawala wa Kizayuni na serikali yenye misimamo mikali ya Benjamin Netanyahu linazidi kuongezeka. Aidha upinzani dhidi ya serikali ya Netanyahu katika jeshi unazidi kuongezeka siku hadi siku.

Tokea kuundwa baraza jipya la mawaziri la Netanyahum jeshi la utawala wa Israel limebainisha wasiwasi kuhusu mawaziri wenye misimamo mikali katika baraza hilo hasa Itamar Ben-Gvir  kiongozi wa chama cha Otzma Yehudit ambaye pia ni Waziri wa Usalama wa Ndani, na  Bezalel Yoel Smotrich, kiongozi wa Chama cha Kidini cha Kizayuni ambaye pia ni Waziri wa Fedha. Jeshi la utawala wa Kizayuni lina wasiwasi kuwa sera zilizotangazwa na viongozi hao wawili wenye misimamo mikali wa baraza la mawaziri zitapalekea kuongezeka changamoto za ndani ya jeshi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na hivyo kusababisha kupuuzwa  vitisho kutoka nje.

Baada ya kuteuliwa katika Wizara ya Usalama wa Ndani, Ben-Gvir  aliongeza wigo wa mamlaka ya polisi katika Ukingo wa Magharibi na wakati huo huo akaanza kuunda jeshi jipya katika wizara hiyo na ambalo linajumuisha askari wa kujitolea wenye itikadi kali za Kizayuni, huku akiwapa silaha walowezi zaidi. Wakati huo huo, Bezalel Yoel Smotrich anayesimamia Wizara ya Fedha, amelipa jeshi hilo lililoanzishwa na Ben-Gvir bajeti ya kutosha sambamba na kuongeza ujenzi wa makazi mapya ya walowezi wa Kizayuni.

Maandamano dhidi ya Netanyahu

Kufuatiliwa siasa hizo na vyama hivyo viwili vilivyo na misimamo mikali ya kufurutu ada katika utawala wa Netanyahu, kumepelekea Jeshi la Israel kuhoji iwapo kweli linaweza tena kuchukuliwa kuwa 'nembo ya umoja' kama ilivyokuwa huko nyuma. Wasiwasi wa jeshi sio tu kuhusu kadhia hiyo bali kama walivyo wapinzani wengine wa Netanyahu, lina wasiwasi kwamba utekelezaji wa kile Netanyahu anakitafsiri kama mageuzi ya mahakama ni jambo linaloweza kuibua changamoto kwa jeshi pia.

Hii ni kwa sababu hitilafu katika uwanja huo ni kubwa na pana kiasi kwamba katika vyombo vya habari na duru za kisiasa za Kizayuni kuna wasi wasi mkubwa kwamba serikali ya sasa ya Israel itakabiliwa na hatima sawa na ile ya serikali za awali za Kizayuni na kusambaratika kabla ya kufikisha umri wa miaka 80. Kwa sababu hiyo, katika kipindi cha wiki chache zilizopita, rais wa utawala haramu wa Israel, Isaac Herzog, ameonya mara kwa mara juu ya matokeo hatari ya kuendelea mizozo ya ndani. Kwa kweli, kile kinachofasiriwa kama mageuzi ya mahakama ni aina ya maelewano kati ya Netanyahu na vyama pamoja na wanasiasa wenye misimamo mikali wanaounda baraza jipya la mawaziri. Lengo la maelewano hayo ni kuhakikisha Netanyahu anafutiwa mashtaka katika kesi zake kadhaa za ufisadi na uhalifu.

Hii ina maana kwamba Netanyahu atafanya kila awezalo kulinda maslahi yake binafsi na inaonekana atashikilia msimamo huo hata kama mwisho wake utakuwa ni vita vya wenyewe kwa wenyewe na kukatisha maisha ya dola la Kiyahudi. Kwa mtazamo huo, mtu anaweza kuelewa wasiwasi wa jeshi kuhusu matokeo ya kile kinachotafsiriwa kama utekelezaji wa mageuzi ya mahakama. Kwa kweli, jeshi la Israel, kama wapinzani wengine, lina wasiwasi kwamba hakutakuwa na chochote kitakachosalia ambacho jeshi litalazimika kukilinda.

342/