15 Aprili 2023 - 20:47
Kufunguliwa mlango wa ubalozi wa Iran mjini Riyadh; hatua mpya ya kutekelezwa makubaliano ya Iran na Saudi Arabia

Milango ya jengo la ubalozi wa Iran mjini Riyadh iliyokuwa imefungwa kwa takribani miaka saba kufuatia kukatwa uhusiano wa nchi mbili, siku ya Jumatano ilifunguuliwa tena na kuashiria azma thabiti ya mataifa haya mawili ya Kiislamu ya kuhuisha tena uhusiano wao wa kidiplomasia.

Katika hatua mpya na katika fremu ya utekelezaji wa makubaliano ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Saudi Arabia ya kuhuisha mahusiano rasmi na ushirikiano wa kidiplomasia, ujumbe wa kiufundi wa Iran Jumatano ya juzi uliwasili mjini Riyadh na kupokewa na maafisa wa Saudia.

Katika taarifa yake, Nasser Kanaani Chafi, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema "ujumbe wa kiufundi" kutoka Iran uliwasili Riyadh Jumatano na Alkhamisi na kukaribishwa na maafisa wa Saudia.

Amesema ujumbe wa Iran utachukua hatua zinazohitajika kwa ajili ya kufungua tena ubalozi mjini Riyadh na ubalozi mdogo mjini Jeddah, na pia mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) katika mji wa Jeddah.

Aliongeza kwamba, juhudi zitafanywa ili kufungua tena ofisi za uwakilishi wa Iran nchini Saudia kabla ya kuanza ibada ya Hija mwaka huu. 

Kan’ani pia alisema kuwa ujumbe wa kiufundi wa Saudi Arabia, ambao ulikuwa umewasili Iran siku ya Jumamosi, jana Alhamisi ulielekea katika mji mtakatifu Mash'had kaskazini mwa Iran kwa lengo la kuandaa mazingira ya kufunguliwa tena ubalozi mdogo wa Saudia katika mji huo mtakatifu.

Hatua hiyo inafuatia mkutano wa wiki iliyopita mjini Beijing kati ya Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran na Saudia, ambao walisisitiza haja ya kutekeleza makubaliano ya nchi mbili ili kuimarisha hali ya kuaminiana na kusaidia kuimarisha usalama katika eneo la Asia Magharibi.

Makubaliano ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Saudia ya kuhuisha tena uhusiano na ushirikiano wa kidiplomasia baina ya pande mbili, linahesabiwa kuwa tukio muhimu kabisa la kisiasa na kidiplomasia katika siku za hivi karibuni katika eneo la Asia Magharibi. Kutokana na tukio hilo kuwa na taathira chanya katika matukio ya eneo limepokewa na kukaribishwa kwa mikono miwili na mataifa jirani. Uhusiano huu mbali na kuunda mashirikiano mapya ya kisiasa na kiuchumi baina ya Iran na Saudia yakiwa mataifa mawili makubwa yenye utajiri wa nishatri ya mafuta na vilevile nchi mbili muhimu za Kiislamu, unaweza pia kuwa na faida na manufaa ya kiuchuumi na wakati huo huo kusaidia pakubwa kueneza amani na uthabiti katika eneo. Aidha hilo linaweza kuwa na msaada mkubwa katika kuipatia ufumbuzi migogoro katika mataifa kama Syria na Yemen.

342/