Tangu Jumanne iliyopita, idadi kubwa ya Wafaransa wamekuwa wakifanya maandamano katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo hususan mjini Paris kupinga mauaji ya polisi wa nchi hiyo dhidi ya kijana mdogo wa Kifaransa mwenye asili ya kaskazini mwa Afrika, "Naël Marzouq". maandamano hayo yamegeuka kuwa vurugu na machafuko makubwa na idadi kubwa ya waandamanaji wametiwa nguvuni huku makumi ya askari usalama na waandamanaji wakijeruhiwa. Magari na ofisi nyingi za umma pia zimechomwa moto. Machafuko hayo makubwa yanaendelea na yameripotiwa kuingia Ubelgiji.
Gari la kijana huyo aliyekuwa na umri wa miaka 17 lilisimamishwa na polisi siku ya Jumanne kwa kukiuka sheria za kuendesha gari katika eneo la "Nanterre" katika viunga vya Paris. Awali idara ya polisi iliripoti kuwa mmoja wa maafisa wake alimpiga risasi kijana huyo kwa sababu alikuwa akijaribu kumgonga, lakini madai hayo yalikadhibishwa na video ya tukio hilo iliyorushwa hewani na kuthibitishwa na shirika la habari la AFP, suala ambalo limeibua maandamano na ghasia kubwa za kupinga ubaguzi na ukatili wa polisi dhidi ya Waislamu na wahajiri wa Kiafrika katika nchi hiyo ya Ulaya. Kulingana na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Ufaransa, afisa wa polisi mwenye umri wa miaka 38 aliyempiga risasi na kumuua kijana huyo ambaye hakuwa na silaha, yuko chini ya ulinzi na anachunguzwa kwa tukio hilo.
Suala muhimu katika muktadha wa mauaji haya ni unyanyasaji na ukatili mkubwa na usio na msingi wa polisi wa Ufaransa. Kwa hakika tunaweza kusema kuwa, mauaji ya kijana huyu mchana kweupe kwa kupigwa risasi na polisi wa Ufaransa na baadaye kuwasilishwa ripoti ya uongo ya tukio ambalo limetafsiriwa kuwa ni "kuwaamerikisha polisi wa Ufaransa" (Americanization of the French police), ni maafa mengine yanayorekodiwa katika faili la polisi wenye hasira ya nchi hiyo, na yamewasha moto wa hasira ya raia na kiu ya kulipiza kisasi. Video ya mauaji ya polisi wa Ufaransa dhidi ya kijana huyo mdogo kwenye mitandao ya kijamii, imezidisha wasiwasi wa Wafaransa juu ya polisi wa nchi hiyo kufuata mienendo ya wa polisi wa Marekani na kufanya ukatili wa kuua raia bila sababu ya maana.