9 Desemba 2023 - 18:59
Safari ya Rais Vladimir Putin wa Russia katika nchi za Imarati na Saudi Arabia

Rais Vladimir Putin wa Russia Jumatano alifanya ziara ya siku moja katika nchi za Imarati na Saudi Arabia ambapo alijadiliana na viongozi wa nchi hizo kuhusiana na uhusiano wa pande mbili na masuala ya kimataifa, vikiwemo vita vya Gaza.

Putin alikuwa hajasafiri katika nchi za Asia Magharibi tangu kuanza janga la Corona. Safari yake ya mwisho katika eneo hilo ilifanyika mwaka  2019. Hata hivyo, Putin amekuwa akikutana na kujadiliana mara kwa mara na viongozi wa Kiarabu kando ya vikao vingine vya  kimataifa.

Safari ya Putin Asia Magharibi na mazungumzo yake na viongozi wa nchi mbili muhimu za Kiarabu katika eneo hili, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu, ina ujumbe na umuhimu mkubwa. Kwanza, licha ya juhudi za nchi za Magharibi hususan Marekani za kuitenga Russia kimataifa na hasa Rais Putin mwenyewe, ziara yake katika nchi hizo za Kiarabu katika Ghuba ya Uajemi inaonesha kuwa hata waitifaki wa kieneo wa Marekani hawazingatii sana matakwa ya Washington katika uwanja huo. Kwa hakika, ziara ya Vladmir Putin katika Umoja wa falme za Kiarabu na Saudi Arabia inaashiria kuwa licha ya juhudi za nchi za Magharibi za kutaka kumtenga Putin, na hasa kutolewa hati ya kimataifa ya kukamatwa kwake na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, lakini bado ana nafasi nzuri katika uga wa kimataifa na anaendelea na safari zake katika nchi nyingine. Mbali na hayo, mapokezi ya kipekee ya Putin katika Umoja wa Falme za Kiarabu, kwa upande mmoja, yanaonyesha umuhimu wa safari yake kwa viongozi wa UAE, na kwa upande mwingine, kutojali viongozi hao maonyo ya Marekani ya kutoimarisha uhusiano wao na Russia.

Hii ni pamoja na kuwa, Wasaudi pia walimkaribisha kwa moyo mkunjufu Putin, jambo ambalo linaashiria mtazamo wa Riyadh kuwa Russia ni nchi yenye ushawishi na satwa kubwa katika uga wa kieneo na kimataifa. Fyodor Lukyanov, Mkuu wa Baraza la Sera za Kigeni na Ulinzi la Russia, anaamini kwamba ziara ya Putin katika nchi mbili muhimu za Ghuba ya Uajemi ni ishara ya wazi kwamba Russia imejiondoa katika kutengwa kimataifa.  Lukyanov anasema : Safari hii inaonyesha lengo la Russia la kuwa na ushawishi katika Mashariki ya Kati na kwamba Umoja wa Falme za Kiarabu na Saudi Arabia, zikiwa washirika wawili wa jadi wa Marekani, zina hamu ya kuleta iwiano katika siasa zao za kigeni. 

Katika upande mwingine, ziara ya Putin pia ina ujumbe mwingine nao ni kwamba, nchi za Kiarabu ambazo ni waitifaki wa Magharibi zinahamu ya kuimarisha ushirikiano na Russia katika masuala yenye maslahi ya pande mbili hususan katika uga wa nishati.

Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Russia, ni wanachama wa kundi la OPEC Plus, ambalo katika miaka miwili iliyopita limechukua maamuzi muhimu ya kupunguza uzalishaji na uuzaji wa mafuta, kinyume na matakwa ya Marekani. Kwa hakika uamuzi wa nchi wanachama wa OPEC Plus kuendelea kupunguza uuzaji mafuta kwenye soko la dunia ulikuwa radiamali ya kukabiliana na uhasama ya Magharibi dhidi ya  Russia na aina fulani ya kuonyesha ushirikiana wao na Moscow. Kwa kuainisha bei ya dola 60 kwa pipa la mafuta ya Russia, Umoja wa Ulaya, G7 na baadhi ya nchi za kambi ya Magharibi kama vile Australia, zilidhani kuwa zingepunguza kwa kiasi kikubwa mapato ya mafuta ya Moscow na hivyo kuidhoofisha katika uwanja huo.