15 Machi 2025 - 21:52
Source: Parstoday
Waumini 80,000 wa Kipalestina washiriki Swala za Ijumaa katika Msikiti wa Al-Aqsa

Waumini wapatao 80,000 wa Kipalestina walishiriki swala ya Ijumaa ya pili ya mwezi mtukufu wa Ramadhani katika Msikiti wa Al-Aqsa jijini Al Quds (Jerusalem) licha ya vizuizi vikali vilivyowekwa na Israel kuwazuia Waislamu kufika katika eneo hilo takatifu.

Idara ya Wakfu wa Kiislamu al-Quds imesema kuwa, idadi hiyo kubwa ya waumini walikusanyika kwa ajili ya Swala ya Ijumaa  huku kukiwa na hofu kubwa ya kuhujumiwa na askari wa utawala wa Kizayuni wa Israel na walowezi wa Kizayuni.

Licha ya vizuizi hivyo, waumini walimiminika kutoka maeneo mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi kuingia kwenye eneo hilo la tatu kwa utakatifu katika Uislamu.

Utawala wa Kizayuni wa Israel umewazuia  vijana wa Kipalestina kutoka Jenin na Tulkarm kuingia katika Msikiti wa Al Aqsa.

Vizuizi hivyo vimewekwa wakati utawala haramu wa Israel unaendeleza ukandamizaji wa Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi. Ukandamizaji huo umesababisha Wapalestina wapatao 40,000 kuhamishwa huku makumi ya wengine wakiuawa shahidi.

Katika taarifa iliyotolewa Ijumaa, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas imelaani vikali vizuizi hivyo na kusema utawala wa Israel unalenga kuvuruga ibada za Waislamu katika mwezi mtukufu wa Ramadhani. Hamas pia imetoa wito wa kuwepo msimamo madhubuti wa nchi za Kiislamu ili kuzuia utawala wa Israel kuendeleza uchokozi wake unaopuuza hisia za Waislamu na maeneo yao matakatifu..

Harakati hiyo pia imehamasisha Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi, Al-Quds, na maeneo mengine yanayokaliwa kwa mabavu kuendelea kutekeleza ibada katika Msikiti wa  Al-Aqsa kama njia ya kukabiliana na vikwazo vilivyowekwa na utawala haramu wa Israel.

Mnamo Machi 6, Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu aliidhinisha vizuizi vikali zaidi kwa lengo la kuwazuia waumini wa Kipalestina kuingia katika Msikiti wa Al-Aqsa wakati wa Swala ya Ijumaa katika Mwezi wa Ramadhani.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha