12 Septemba 2025 - 12:20
Hakim: Kimya mbele ya uvamizi wa Israel hakikubaliki

Sayyid Ammar Hakim amesema kuwa ujasiri wa hali ya juu na dharau ya wazi ya utawala wa Kizayuni katika kuvamia nchi za Kiarabu na Kiislamu, na kutenda jinai za kila siku dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza, Ukingo wa Magharibi, Syria, Lebanon, Yemen, Iran na Qatar ni jambo ambalo kimya dhidi yake hakikubaliki.

Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Sayyid Ammar Hakim, katika sherehe kuu ya Maulidi ya Mtume Mtukufu Muhammad (s.a.w.w) iliyoandaliwa Baghdad kwa kuhudhuriwa na viongozi wa juu wa Iraq, alitoa wito wa kutumia tukio hili kama fursa ya kuwekeana ahadi ya kujenga Iraq iliyoungana na yenye nguvu.

Kiongozi wa Harakati ya Hikma ya Kitaifa ya Iraq, katika hotuba yake, alitangaza mradi wa kitaifa kwa jina la "Mpango wa Kinabii wa Iraq”, akisisitiza kuwa mpango huu umejengwa juu ya misingi ya haki, umoja, kuhudumia watu, na kuinua hadhi ya binadamu. Alieleza kuwa lengo ni kuibadilisha Iraq kuwa nchi inayounganisha Mashariki na Magharibi, na kuwa jukwaa la mazungumzo ya kikanda na kimataifa badala ya uwanja wa mizozo na migogoro.

Amehimiza haja ya umoja wa maneno na msimamo mmoja mbele ya hatari na changamoto zinazowakabili wote bila kujali madhehebu au kabila, na kutoa wito wa kubadilisha maadhimisho ya kuzaliwa kwa Mtume (s.a.w.w) kuwa fursa ya umoja, upya wa taifa, na kuinuka kwa Iraq na wananchi wake.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Sayyid Ammar Hakim alikemea ujasiri wa hali ya juu wa utawala wa Kizayuni katika kushambulia nchi za Kiarabu na Kiislamu, pamoja na kutenda jinai za kila siku dhidi ya watu wa Gaza, Ukingo wa Magharibi, Syria, Lebanon, Yemen, Iran na Qatar, na akasisitiza kuwa kimya mbele ya hali hiyo hakikubaliki. Aliongeza kuwa Iraq na watu wake wapo pamoja na waliodhulumiwa na wanaoteseka.

Kuhusu uchaguzi unaotarajiwa kufanyika nchini Iraq, alisema kuwa kila upande una haki ya kuwaelekeza wafuasi wake kulingana na kile unachoona kuwa ni kwa maslahi ya taifa, lakini hili halipaswi kuvuruga umoja na mshikamano wa kitaifa.

Ammar Hakim alieleza kuwa umoja wa kitaifa ni mstari mwekundu, na hakuna mtu au kundi lolote ambalo linapaswa kuruhusiwa kuuvuka au kuupuuza mstari huo, kwa sababu yoyote ile au kwa sababu ya maslahi binafsi.

Aidha, alitoa wito wa ushiriki mpana, wenye tija na wa uelewa katika uchaguzi, akasisitiza umuhimu wa kujenga tena imani kati ya serikali na wananchi kupitia kupambana na ufisadi na kutekeleza mageuzi ya kweli. Alisisitiza kwamba ni lazima dunia ionyeshwe kuwa wa_Iraq wanaweza kushindana kwa heshima na kuonesha taswira chanya ya Taifa lao.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha