Kwa Mujibu wa Ripoti ya Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA-: Mwenyekiti na Kiongozi Mkuu wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) , Sheikh Dk. Al-Had Mussa Salum Al-Naqshbandi, ametoa ufafanuzi wa kina na maridhawa juu ya neno "UNABII" linalotumika sana Nchini Tanzania kwa baadhi ya Watu wanaosikikika wakijiita au wakiitwa Nabii, au Nabii Mkuu. Ni suala la kimantiki na lilisopingika kwamba ufafanuzi huu wa kielimu na maarifa alioutoa, unatosha kabisa kuondoa utata uliopo kuelekea matumizi ya neno Unabii au Utume baina ya Waislamu na Wakristo, na hatimaye kuendelea kuishi pamoja kwa upendo, maridhiano na amani, na kujenga Taifa moja la Tanzania.
Aakifafanua juu ya matumizi ya neno Unabii amesema: "Sisi kama Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania, tunasisitiza kuishi kwa Maridhiano na Amani, hivyo yanapotokea mambo kama haya tunatakiwa kuyazungumzia na kuyatatua kwa Maridhiano na Amani, na kwa kuheshimu kila mtu na Dini yake".
Wakristo wanaposema, au tunaposikia ikisemwa, au anapoitwa mtu kuwa ni Nabii au Nabii Mkuu, anaitwa hivyo kwa Istilahi ipi?! Hili ndio swali la msingi kujiuliza?. Anaitwa hivyo kwa Istilahi yetu sisi Waislamu au kwa istilahi yao hao ndugu zetu Wakristo?!. Kwa sababu katika suala la UNABII kila watu wana Istilahi zao.
Sisi kama Waislamu tunazo istilahi zetu kuhusiana na neno Unabii na Utume.Kwetu sisi Waislamu kuna Nabii, kuna Rasulu (Mtume). Tunaposema Nabii katika Uislamu tunamaanisha Mtu aliyepewa Ujumbe wa Unabii (Utume), lakini hajakalifishwa ule ujumbe aliopewa kuufikisha kwa watu wengine, lakini ni Nabii, kama vile: Nabii Adam (a.s). Yeye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu lakini alichopewa hajalazimishwa (hajakalifishwa) kukipeleka kwa wengine.
Kisha kuna Rasulu (au Rasuli), kwa Maana Mjumbe. Mjumbe (au rasulu), ni mtu aliyepewa Utume, halafu akalazimishwa (akapewa wajibu wa) kuufikisha ule ujumbe kwa wengine. Kwa hiyo kuna mwingine anavyote hivyo, yaani ni Nabii na wakati huo huo ni Mjumbe (Rasulu au Rasuli).
Kwa mantiki hiyo, sisi Waislamu, katika Istilahi zetu, na itikadi zetu na imani zetu za Kiislamu zilivyo, hakuna Nabii wala Mtume (wala Mjumbe) baada ya Mtume wetu Muhammad (saww).
Lakini, tunaona na tunasikia kwa wenzetu Wakristo siku zote wakisema kuwa kuna manabii, kuna mitume, kuna manabii wakuu. Sisi tunachotakiwa kukizingatia ni hiki kwamba: Hayo wanayoyasema wao, yako kwenye vitabu vyao, na wala hayapo katika vitabu vyetu Waislamu. Na kwa kuwa yapo katika vitabu vyao, inabidi tuwaache na vitabu vyao, natujue tu kwamba kwao kuna manabii na mitume. Ama tukija kwetu sisi Waislamu, hakuna nabii wala mtume baada ya Mtume wetu Muhammad (s.a.w.w).
Kwahiyo, hili ni suala rahisi tu la kueleweshana na kuhakikisha kuwa tunayafahamu mambo haya kwa utaratibu uliokuwa mzuri, ili tuweze kuishi pamoja kwa Maridhiano na Amani na kwa kuheshimu vizuri.
Maana ya Unabii na Utume ndani ya Biblia:
Kwa mfano: Katika Biblia tukisoma Waifeso 4: 11 inasema kuhusu Yesu: "Yeye ndiye aliyewapa watu vipawa, wengine kuwa mitume, wengine kuwa manabii, wengine kuwa wainjilisti, na wengine kuwa wachungaji na walimu".
Pia, ukitizama Waefeso 4, katika Biblia ya Lugha ya Kiarabu, pia imeandikwa hivyo kama kiarabu ambapo maana yake ni kama ilivyo andikwa kwa Kiswahili. Kwa kiarabu imeandikwa hivi:
"وَهُوَ أَعْطَى الْبَعْضَ أَنْ يَكُونُوا رُسُلًا، وَالْبَعْضَ أَنْبِيَاءَ، وَالْبَعْضَ مُبَشِّرِينَ، وَالْبَعْضَ رُعَاةً وَمُعَلِّمِينَ" (أفسس: 4: 11).
Kwa hiyo, suala la UNABII unaotajwa kwa ndugu zetu Wakristo, ni UNABII kwa Mujibu wa vitabu vyao. Hivyo sisi kama Waislamu, hatuna shida kwa Wakristo juu ya wao kumuita mtu nabii au nabii mkuu, kwa sababu hayo sio katika zetu, bali hayo ni kwa mujibu wa imani zao.
Na Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania, inajumuisha watu wa Imani tofauti tofauti, na tunaishi kila mtu na Imani yake.
Na ukitizama pia Matayo 23: 34 imeandikwa namna hii:
"Kwa sababu hiyo nawapelekea manabii na wenye hekima na walimu...".
Na kwa Biblia ya Lugha ya Kiarabu pia imeandikwa hivyo hivyo kama ifuatavyo:
"لِذلِكَ هَا أَنَا أُرْسِلُ إِلَيْكُمْ أَنْبِيَاءَ وَحُكَمَاءَ وَكَتَبَةً...." (إنجیل متی 23: 34).
"Kwa sababu hiyo nawapelekea manabii na wenye hekima na walimu...".(Matayo 23: 34).
Kwa hiyo, kuna tofauti katika Istilahi ya UNABII baina yetu Sisi Waislamu kwa wenzetu Wakristo. Kwa Wakristo wao UNABII unachukuliwa kuwa ni Wanafunzi wa Yesu, wafuasi wa Yesu, Watumishi wa Yesu, waandishi wa Yesu.
Itikadi ya Dini ya Kiislamu kuhusu Unabii na Utume:
Kwetu kama Waislamu hili haliwezi kamwe kutukwaza, kwa sababu hilo ni kwa mujibu wa Imani yao na itikadi yao. Kwetu Sisi Waislamu, hakuna Nabii wala Mtume baada Mtume wetu Muhammad (s.a.w.w).
Tizama katika Surat al_Ahzab: Aya ya 40, Mwenyezi Mungu anasema hivi:
"مَّا كَانَ مُحَمَّدٌ أَبَا أَحَدٍ مِّن رِّجَالِكُمْ وَلَـٰكِن رَّسُولَ اللَّـهِ وَخَاتَمَ النَّبِيِّينَ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمًا"
“Hakuwa Muhammad baba wa yeyote miongoni mwa wanaume wenu, lakini ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na ni Mwisho wa Manabii. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi zaidi kwa kila kitu".
Hii ndio Imani na Itikadi ya Dini ya Kiislamu.
Hivyo, kwa Iman za wenzetu, watu wakiitwa nabii au nabii, hiyo ni kwa mujibu wa imani zao na Dini yao, na Sisi Waislamu tuna Dini yetu na Imani yetu.
Na Jumuiya yetu, inajumuisha watu wenye Dini mbalimbali na wengine hata hawana Dini, wengine ni mabudha n.k. Hatufanyi Dini mseto katika Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania. Tunaishi kwa kuheshimiana na imani zetu, na tunahitajiana katika maisha, ukienda Hospital wewe ni Muislamu, hausemi nataka kutibiwa na daktari Muislamu, na hivyo hivyo Mkristo hasemi nataka kutibiwa na daktari Mkristo, au hatusemi nataka kufundishwa shuleni na Mwalimu Muislamu kwa kuwa wewe ni Muislamu au Mwalimu Mkristo kwa kuwa wewe ni Mkristo, kila mtu anaishi kwa imani yake, na tunaishi pamoja kwa maelewano mazuri, kwa kupendana na kushirikiana, na kujenga Taifa moja la Tanzania.
Na Mwenyezi Mungu Ndiye Walii wa Taufiki.
Na Amani ya Mwenyezi Mungu na Baraka zake ziwe juu yenu.
Your Comment