26 Machi 2025 - 15:25
Source: Parstoday
Makumi ya wafanyakazi wa UN wanaondoka Gaza, Israel yazidisha mauaji

Kufuatia mashambulizi ya Israel dhidi ya kambi za Umoja wa Mataifa katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na kuuawa wafanyakazi watano wa shirika hilo la kimataifa, makumi ya wafanyakazi wa kimataifa wa Umoja wa Mataifa katika Ukanda wa Gaza wanaondoka eneo hilo kutokana na wasiwasi wa mashambulizi ya Israel.

Umoja wa Mataifa ulitangaza Jumatatu iliyopita kwamba unapanga kupunguza idadi ya wafanyikazi wake huko Gaza kufuatia duru mpya ya mashambulio ya Israel.

Umoja wa Mataifa una wafanyakazi zaidi ya 13,000 katika Ukanda wa Gaza, wengi wao wakiwa Wapalestina, wanaofanya kazi muhimu kama vile madaktari, wauguzi, madereva na kazi nyingine.

Zaidi ya wafanyakazi 250 wa UN wameuawa na Israel katika kipindi cha miezi 15 iliyopita.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, anasema hali imekuwa ya hatari kiasi kwamba anapanga kupunguza wafanyakazi wa kimataifa wanaofanya kazi Gaza kwa takriban theluthi moja, kwa msingi huo, wafanyakazi karibu 30 wa UN wataondoka Gaza kwa kuhofia usalama wao.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric amewaambia waandishi wa habari huko New York siku  kwamba: "Wiki iliyopita, Israel ilifanya mashambulizi makubwa huko Gaza na kuua mamia ya raia, ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, na pia imezuia misaada ya kibinadamu kuingia eneo hilo tangu mapema mwezi huu wa Machi." 

Makumi ya wafanyakazi wa UN wanaondoka Gaza, Israel yazidisha mauaji

Afisa huyo wa wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa amesema: "Katibu Mkuu wa UN analaani vikali mashambulizi haya na anatoa wito wa kufanyika uchunguzi kamili na huru kuhusu tukio hilo."

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha