5 Aprili 2025 - 23:32
Source: Parstoday
Mufti wa Oman akosoa vikali kimya kinachoonyeshwa mbele ya jinai za Israel dhidi ya Ghaza

Mufti Mkuu wa Oman, Sheikh Ahmed al-Khalili, amekosoa vikali kimya kinachoonyeshwa mbele ya jinai za kinyama zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Ghaza.

Sheikh Al-Khalili ameandika katika ukurasa wake rasmi wa Mtandao wa X: "kimya hiki kizito kinachoonyeshwa mbele ya kiwango hiki cha unyama unaofanywa bila huruma kinamaanisha nini? Hakuna tena mshipa wowote wa uhai uliosalia ndani ya mwili wa Umma wa Kiislamu wa kuweza kututa kuashiria uhai? Au tukubali kwamba hata dhamiri hai na zilizo macho za utu nazo pia zimezimika?"

Wakati huohuo, msemaji wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS, Sami Abu Zuhri ametahadharisha kuwa, kimya ambacho hakijawahi kushuhudiwa kinachoonyeshwa na nchi za Kiarabu na Kiislamu kimeupa uthubutu zaidi adui mzayuni wa kuendelea kutekeleza mipango yake angamizi dhidi ya watu wa Palestina katika Ukanda wa Ghaza.

Abu Zuhri ameongeza kuwa, kinachojiri Ghaza si mashambulizi tu dhidi ya Hamas, bali pia ni njama ya wazi kabisa ya kufuta kikamilifu uwepo wa Wapalestina.Msemaji wa Hamas amebainisha kuwa, lengo la utawala wa Kizayuni la kufanya jinai hizo za mauaji ya kimbarii ni kuigeuza Ghaza kuwa kambi kubwa ya mahabusu isiyo na hata hali ya chini kabisa ya maisha, ili kuwafanya Wapalestina walazimike kulihama eneo hilo.

Mnamo Machi 18, utawala wa Kizayuni wa Israel ulianzisha tena vita vya kinyama na mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Ghaza na kuvunja kikamilifu usitishaji mapigano uliodumu kwa miezi miwili kufuatia makubaliano uliyofikia na harakati ya Hamas kwa upatanishi wa serikali iliyopita ya Marekani, Qatar na Misri. 

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Ghaza, Wapalestina wapatao 1,249 wameuawa shahidi na wengine 3,022 wamejeruhiwa tangu utawala wa Kizayuni ulipoanzisha tena mashambulio hayo ya kinyama na mauaji ya kimbari dhidi ya Ghaza.../

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha