Kwa mujibu wa shirika la habari la Ahlul-Bayt (a.s) - ABNA - katika mkutano wa kitaalamu uliofanyika katika Shule ya Kiislamu ya Imam Kadhim (a.s) mjini Qom, kwa kushirikisha wanazuoni na wasomi mashuhuri kutoka nchi mbalimbali, Ayatollah Reza Ramazani, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (a.s), alizungumza na kufafanua vipengele vya maarifa na ustaarabu wa Kiislamu. Alisema:
“Katika Uislamu tuna misingi miwili chanya na miwili hasi ambayo imeathiri mfumo wetu wa maarifa. Misingi chanya ni heshima ya binadamu katika nyanja zote za uwepo, na haki au uadilifu. Kinyume na mtazamo wa Magharibi ambao unaona heshima kama jambo la kukabiliana na hali, Uislamu unaiona heshima kama msimamo wa msingi. Katika muktadha wa mabadiliko ya kijamii, uadilifu ni msingi mkuu ambao umekuwa ndoto ya manabii wote wa Mungu, na ni asili ya mwanadamu."
Aliendelea kueleza kuwa misingi miwili hasi ni kufanya dhulma na kudhulumiwa, ambayo inapaswa kuelezwa kwa usahihi na mashaka yanayozunguka suala hilo kujibiwa.
Historia ya Majaribio ya Kuondoa Dini
Ayatollah Ramazani alitaja kuwa kuna aina mbili za kukabiliana na dini katika historia: kuiondoa kabisa na kuipunguza hadi kwenye mipaka finyu. Katika zama za Renaissance, akili ya wahyi iliondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na akili ya kujitegemea, hadi akili ikawa mpinzani wa dini. Katika Umoja wa Kisovyeti, kwa zaidi ya miaka 70 walijaribu kuondoa dini, na leo hii pia, mifumo ya Kimagharibi inajaribu kuipunguza dini. Hata hivyo, licha ya juhudi hizo, leo tunaona kurejea kwa dini hata katika mazingira ya kitaaluma, jambo linalothibitisha kushindwa kwa mradi wa kuiondoa dini.
Mapinduzi ya Kiislamu na Fursa za Leo
Akisisitiza athari ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, alisema:
“Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Waislamu walipata fursa bora zaidi katika historia yao. Wengine waliamini kuwa mapinduzi ya kidini hayawezekani, na kwamba mapinduzi lazima yawe ya kisekula au ya kiliberali. Lakini Mapinduzi ya Kiislamu yaliyoongozwa na Imam Khomeini (r.h) yalibatilisha dhana hiyo na kuleta mabadiliko makubwa duniani. Ni Uislamu pekee ulioweza kujitokeza kimataifa na kupinga mfumo wa kidhalimu.”
Wito kwa Vyuo vya Kidini (Hawza)
Ayatollah Ramezani alieleza kuwa:
“Leo vyuo vya kidini vina fursa ya kipekee ambayo haijawahi kutokea kabla. Ni lazima tuweze kuitambulisha dini ya Uislamu duniani kwa kutumia lugha ya kimataifa. Bila shaka, tutaweza kufanikiwa katika njia hii. Magharibi leo inakumbwa na migogoro mikubwa ya fikra, mtazamo na vitendo. Katika uchumi, asilimia 90 ya utajiri wa dunia inamilikiwa na chini ya asilimia 10 ya watu, huku watu bilioni 2 wakiteseka na utapiamlo. Hii ni 'haki ya kiuchumi' ambayo zama za kisasa ziliahidi, lakini zimeshindwa kuitekeleza.”
Changamoto za Sasa: Mitandao, Islamu ya Kiliberali, na Islamu ya Takfiri
Alihimiza matumizi mazuri ya mitandao ya kijamii kuutambulisha Uislamu, lakini pia akaonya kuhusu:
- Jaribio la kuwasilisha Uislamu wa kiliberali na kuondoa aya za jihadi kutoka kwenye Qur’ani.
- Kujitokeza kwa Uislamu wa Takfiri (wenye misimamo mikali) unaolenga kueneza chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia).
- Vyuo vya kidini vinapaswa kukemea upotoshaji wa dini kama vile ule wa zama za Bani Umayyah na Bani Abbas.
Ujumbe wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi
Ramazani alieleza kuwa katika ujumbe wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi, kumeangaziwa dhana mbili muhimu:
- Fiqhi ya kujenga umma
- Uislamu unaojenga ustaarabu
Alihitimisha kwa kusema kuwa:
“Lazima tuweke mkazo katika kurudi kwenye kiini cha dini, tukizingatia vipengele vyote vya uwepo wa mwanadamu. Qur’ani imezingatia upeo huu wa kina. Fiqhi peke yake si dini yote — dini ina vipengele vingine muhimu kama vile maadili na itikadi ambavyo ni muhimu kwa kumjenga muumini wa kweli.”
Your Comment