Rais Abdul Fatah al Sisi wa Misri leo anaanza ziara yake ya siku mbili nchini Ujerumani. Rais huyo anatarajiwa kupokelewa na Rais Joachim Gauck wa Ujerumani kabla ya kukutana na Kansela Angela Merkel. Al Sisi ni kiongozi mwenye utata kutokana na ukiukaji wa haki za binaadamu unaofanyika chini ya utawala wake wakati huo huo anahesabiwa kama mshirika na mataifa ya magharibi katika vita dhidi ya ugaidi wa Waislamu wa itikadi kali, ambapo Misri ni moja kati ya nchi zenye waislamu wengi wenye itikadi kali.
Spika wa bunge la Ujerumani Bundestag Norbert Lammert amefuta mkutano wake na mgeni huyo wa taifa kutokana na kile alichokitaja kuwa ni kukandamizwa kwa upinzani nchini Misiri na kutolewa kwa idadi kubwa ya hukumu za vifo nchini humo. Yumkini ziara hiyo ya al Sisi nchini Ujerumani imepelekea kuahirishwa uamuzi wa kumhukumu kifo raisi aliyekuwa kabla yake Mohamed Mursi na mahakama ya Cairo hapo jana, Musri alitolewa madarakani kwa nguvu za kijeshi zilizoongozwa na rais wa sasa wa Misri Abdul Fatah Al sisi.