Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Kimataifa la AhlulBayt (a.s) -ABNA- Ayatollah Reza Ramezani, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya AhlulBayt (a.s), alitembelea makao makuu ya Jumuiya ya Kitaifa ya Maimamu wa Misikiti na Maulamaa wa Senegal, ambapo alikutana na kufanya mazungumzo na Sheikh Omar Jane, Rais wa Jumuiya hiyo.
Umoja wa Kiislamu na Mamlaka ya Kiulimwengu
Ayatollah Ramezani alieleza kuwa: “Tuna furaha kuwa hapa. Sote ni ndugu; matatizo yenu ni matatizo yetu. Tunapaswa kuelekea kwenye kuundwa kwa ‘Ummati wa Kiislamu’. Pale umma wa Kiislamu unapotimia, hutoa mamlaka na nguvu kwa Waislamu.”
Maendeleo ya Iran na Nguvu ya Elimu
Kuhusu maendeleo ya Iran, alisema: “Imam Khomeini (r.a) alitufundisha somo kubwa kwamba tunaweza kuijenga nchi yetu wenyewe. Leo, tumepiga hatua kubwa kielimu na katika nyanja nyingine. Kabla ya Mapinduzi, nafasi ya kielimu ya Iran duniani ilikuwa ya 57, sasa tuko nafasi ya 17, na katika baadhi ya nyanja tuko ndani ya tano bora duniani. Hii ndiyo nguvu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, lakini maadui hawataki tuendelee kielimu.”
Uislamu ni Dini ya Rehema – Hatutengenezi Mabomu ya Nyuklia
Ayatollah Ramezani alisisitiza kuwa: “Sisi hatufanyi juhudi yoyote ya kutengeneza bomu la nyuklia. Mtume wetu ni Mtume wa rehema, naye alisema kuwa amebebeshwa ujumbe wa rehema. Dunia inapaswa kuwashughulikia wale wenye silaha za nyuklia, lakini maadui hutaka kutumia nguvu daima.”
Pendekezo kwa Senegal: Jengeni Imani na Elimu ya Vijana
Kuhusu Senegal, alisema: “Senegal sasa imeanza kujitambua. Wote tunapaswa kusaidia nchi hii kustawi katika imani na elimu. Tumewaambia viongozi wa Senegal kuwa wanaweza kuwatuma vijana wao Iran kujifunza. Tunapaswa kuwafundisha vijana kuwa tuna uwezo, hatuhitaji wengine watufanyie maamuzi.”
Dini na Maadili: Mustakabali wa Binadamu upo katika Uislamu
Ayatollah Ramezani alisisitiza kuwa: “Mustakabali wa mwanadamu umo katika Uislamu. Qur'an inasema: 'Islamu hutukuka wala hautukuzwi.' Uislamu unatufundisha maarifa, hali ya kiroho na majukumu. Kadri roho inavyoinuka, ndivyo wajibu unavyoongezeka. Lazima tuhifadhi hali ya kiroho ya vijana wetu.”
Ubepari na Ukosefu wa Haki: Waislamu Wapaswa Kushikamana
Akiashiria mafundisho ya Kiislamu kuhusu usawa na huruma, alisema: “Qur’an inasema tuwe na nguvu katika kila hali. Hatupaswi kuruhusu taifa lolote la Kiislamu kutendewa dhulma. Mtume alitufundisha kuwa dua zetu ziwaguse wote: ‘Ewe Mungu, mponye kila mgonjwa’, ‘mjalie riziki kila fakiri’. Hata asiyekuwa Mwislamu akihitaji msaada na unaweza kumsaidia lakini hukufanya hivyo — basi hujakuwa Mwislamu wa kweli.”
Sheikh Omar Jane: Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni Kielelezo cha Fahari kwa Umma
Katika mkutano huo, Sheikh Omar Jane alisema: “Uwepo wenu umetufurahisha sana. Ni fahari kubwa kwetu kukutana nanyi.” Alikumbusha kuwa Mtume Muhammad (s.a.w.w) alihimiza sana umoja wa Kiislamu, na kwamba leo zaidi ya wakati mwingine wowote, umoja huo ni muhimu.
Aliongeza kuwa: “Maimamu wa misikiti wana nafasi muhimu katika kuwaongoza watu. Maulamaa wa Senegal wapo kwenye vyombo vya habari, vyuo vikuu na mashule, wakielekeza watu kwenye Uislamu na maisha ya Kiislamu. Kwa sababu vyombo vya habari vya kisasa mara nyingi hupingana na maadili ya dini.”
Sheikh Omar aliendelea: “Ikiwa hatutawalea watoto na wanawake wetu kwa misingi ya Kiislamu, vyombo vya habari vya uharibifu vitawapotosha. Familia ni msingi wa jamii, na mustakabali wetu unategemea afya ya kiakili na kidini ya vijana.”
“Iran Ipo Ndani ya Nafsi Zetu”
Akiainisha nafasi ya Iran katika ulimwengu wa Kiislamu, alisema: “Iran imeleta mapinduzi makubwa yenye msingi wa haki, yaliyolipa Uislamu heshima. Tangu ushindi wa Mapinduzi, Iran ipo ndani ya roho na maumbile yetu.”
Alimaliza kwa kusema: “Sisi tunafanya kazi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, naye ameahidi kuwapa thawabu wahudumu Wake. Iran ni nchi ya wanavyuoni wakubwa na yenye msimamo thabiti dhidi ya madhalimu. Tunatarajia mahusiano yetu na ninyi yazidi kuimarika kila siku.”
Ukumbi wa Jumuiya ya Maulamaa wa Senegal Wapambwa kwa Jina la Imam Khomeini (r.a)
Mwisho wa ziara hiyo, Ayatollah Ramezani alimpa Sheikh Omar Jane pete yake binafsi. Sheikh Omar alitaka ukumbi mmoja wa jumuiya hiyo upewe jina la Ayatollah Ramezani, lakini Ayatollah alikataa, akapendekeza ukumbi huo upewe jina la Imam Khomeini (r.a) katika kuelekea kumbukumbu ya kifo chake.
Your Comment