Chaneli hiyo imeelezea kile ilichokiita "mapigano makali" wakati wanajeshi wa Israel walipojaribu kusonga mbele, huku ripoti za mitandao ya kijamii kuhusiana na matukio huko Ghaza zikiashiria kuuawa na kujeruhiwa wanajeshi kadhaa wa utawala huo wa kizayuni.
Chaneli maarufu ya habari ya Roya News imeripoti leo kuwa, mwanajeshi mmoja wa Israel ameuawa na wengine 11 wamejeruhiwa katika mapigano makali yaliyojiri kwenye kitongoji cha Al-Zeitoun kilichoko katika Mji wa Ghaza. Kwa mujbu wa chaneli hiyo, wanajeshi wengine wanne wametoweka wakiwa hawajulikani waliko.
Duru za kisiasa za Israel zimeeleza wasiwasi zilionao kuwa huenda wapiganaji wa Muqawama wa Palestina wamewakamata mateka wanajeshi wanne wakati wa mapigano hayo.
Kutokana na picha na taswira zinazoonyesha nyendo nyingi za helikopta, miale ya moto na milio ya mapigano makali, wachambuzi wanasema jeshi la Israel linaweza kuwa limeanzisha kile kiitwacho "Itifaki ya Hannibal", inayoruhusu kuwaua askari wake ili kuzuia wasikamatwe mateka.
Hayo yanajiri baada ya Brigedi za Izzuddinul-Qassam, tawi la kijeshi la harakati ya ukombozi wa Palestina ya Hamas, kutoa indhari kali kupitia msemaji wake Abu Obeida kwamba mipango ya Israel ya kuamua kuikalia kwa mabavu kikamilifu Ghaza itakuwa matokeo mabaya kwa utawala huo wa kizayuni na kwamba hali ya mapigano inazidisha uwezekano wa askari wa Israel kukamatwa mateka.
Abu Obeida ametahadharisha pia kuwa, mateka wa Israel watasalia kwenye maeneo ya mapigano wakikabiliwa na hatari sawa na inayowakabili wapiganaji wa Kipalestina.
"Mateka wowote watakaouawa katika mashambulizi ya Israel watatangazwa hadharani kwa majina, picha na vyeti vyao vya kifo," amesisitiza msemaji huo wa al-Qassam.../
Your Comment