5 Desemba 2025 - 15:12
Umoja wa Waislamu na kuunga mkono Iran kama mstari wa mbele wa kulinda Quds ni jambo la lazima

Mwanafikra mashuhuri wa Algeria amesisitiza kuwa umoja wa Waislamu, kuacha misimamo ya chuki za kimadhehebu na kuunga mkono Iran kama ngome ya mbele ya kulinda Quds (Msikiti wa Al-Aqsa) na Umma wa Kiislamu ni jambo la lazima, na kwamba mataifa pamoja na wanazuoni wa Kiislamu wanapaswa kusimama bega kwa bega na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nyanja za vyombo vya habari, siasa, utamaduni na usalama.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Dkt. Yahya Abuzakariya, mwanafikra mashuhuri kutoka Algeria, katika Wabinaar wa pili wa Kimataifa wenye mada: “Iran ya Kiislamu; Uwanja wa Heshima ya Uislamu katika mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni” ulioandaliwa na Jumuia ya Kimataifa ya Qadimun, alisema akirejea njama nyingi za Magharibi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa: Tangu ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hadi leo, Iran daima imekuwa shabaha ya maelfu ya njama kutoka kwa madola ya Magharibi na Uzayuni wa Kimataifa. Hata hivyo ni nchi iliyoweka uwezo wake wote katika kuwaunga mkono wanyonge na kuwasaidia wadhulumiwa. Kwa misingi ya uamuzi wa kifiqhi na kimkakati wa Imamu Khomeini (rehma za Mwenyezi Mungu zimshukie), Iran imeinua bendera ya kutetea Palestina na harakati za mapambano katika eneo.

Akaongeza kuwa: Ilitarajiwa Umma wa Kiislamu na wanazuoni wa Kiarabu waunge mkono misimamo hii ya kimsingi ya Iran, lakini cha kusikitisha ni kwamba baadhi ya fatwa na mikondo ya kidini ilitumika kuivuruga Iran ya Kiislamu, ilhali vyanzo hivyo vya kisheria vilitumika kuhalalisha mahusiano na utawala wa Kizayuni.

Abuzakariya alisisitiza kuwa: Iran katika kipindi cha zaidi ya miongo minne imebeba gharama nzito kwa ajili ya kutetea malengo ya Kiislamu. Wairani wangeweza, kama baadhi ya nchi za eneo hili, kuungana na Magharibi, lakini wao waliinua Qur’ani, Uislamu na Mtume Mtukufu (s.a.w.w) na kusimama pamoja na mataifa yaliyodhulumiwa katika nyanja zote za kuitetea dini ya Uislamu.

Mwanafikra huyo wa Algeria, akitaja kuwepo kwa miradi miwili ya “mapambano” na “maelewano” katika ulimwengu wa Kiarabu, alisema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa katika safu ya mapambano na bado inaendelea kupigania ushindi wa wanyonge. Ndiyo maana Marekani na madola yote ya Magharibi kwa kushirikiana na utawala wa Kizayuni yamekusanyika dhidi ya nchi hii, lakini Iran, kwa uongozi wenye hekima na ujasiri wa Kiongozi wa Mapinduzi, Ayatollah al-Udhma Sayyid Ali Khamenei (Mungu amlinde), imesimama kwa nguvu na heshima dhidi ya mashinikizo yote.

Akaongeza kuwa: Ayatollah Khamenei wameweka wazi kuwa taifa la Iran halikubali fedheha wala halikubali udhibiti wa maadui. Huu ndio mkondo wa Ashura unaowaita watu huru kutetea heshima yao.

Abuzakariya aliendelea kwa kusema: Ulinzi wa Iran ya Kiislamu ni wajibu wa kisheria (wa kidini) na pia ni haja ya kimkakati ya Umma wa Kiislamu. Kuanguka kwa Iran – jambo ambalo kamwe halitawezekana kutokana na uwepo wa taifa lenye busara, uongozi wa hekima na wanamapinduzi – kungemaanisha kusambaa kwa Uzayuni, kuiweka dunia ya Kiislamu chini ya udhibiti wa Marekani, na kusukuma mbele mradi wa “Israel Kubwa.”

Akasema kwa msisitizo: Umoja wa Waislamu, kuacha chuki za kimadhehebu na kuunga mkono Iran kama mstari wa mbele wa kulinda Quds na Umma wa Kiislamu ni jambo la lazima, na mataifa pamoja na wanazuoni wa Kiislamu wanapaswa kusimama upande wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika vyombo vya habari, siasa, utamaduni na usalama.

Mwisho wa hotuba yake alisema: Kwa zaidi ya miaka arobaini, Iran imeipatia dunia ya Kiislamu mafanikio makubwa, na uwepo wake katika ulingo wa kikanda na kimataifa ni hitaji la lazima kwa maendeleo na heshima ya Umma wa Kiislamu. Leo hii ni wajibu wa Waislamu wote kuisimamia Iran ya Kiislamu dhidi ya maadui wa Uislamu.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha