Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- kitendo cha hivi karibuni cha kibaguzi kilichofanyika katika mji wa Stockholm, mji mkuu wa Uswidi kaskazini mwa Ulaya, kimeonesha tena kuwa wimbi la chuki dhidi ya Uislamu Magharibi limevuka kiwango cha matusi ya kimaandishi au ya ishara, na sasa limeingia katika hatua ya vurugu na vitisho vya moja kwa moja. Katika tukio hilo, nakala ya Qur’ani Tukufu iliyokuwa imefungwa kwa mnyororo kwenye uzio wa lango la kuingilia Msikiti Mkuu wa Stockholm iligundulika ikiwa na mashimo sita ya risasi.
Juu ya Qur’ani hiyo, kulikuwa na ujumbe wa vitisho uliobeba kauli: “Asanteni kwa ziara yenu, lakini sasa ni wakati wa kurudi nyumbani,” uliandikwa kwa lugha ya Kiarabu na Kiswidi; ujumbe ambao kwa uwazi kabisa uliwalenga Waislamu na unaashiria nia ya wazi ya mhusika au wahusika wa tukio hilo kuwatisha na kuwafukuza Waislamu kutoka katika nafasi ya umma.

Viongozi wa Msikiti Mkuu wa Stockholm walilitaja tukio hili kuwa ni shambulio la moja kwa moja dhidi ya uhuru wa dini na usalama binafsi wa Waislamu. “Mahmoud al-Halfi,” mkurugenzi wa kituo kinachohusiana na msikiti huo, alisisitiza kuwa tukio hili limetokea katika mazingira ya ongezeko la uchochezi dhidi ya Uislamu, ubaguzi wa rangi na mgawanyiko wa kijamii nchini Uswidi, na haliwezi kuchukuliwa kama tukio la mtu mmoja binafsi lisilo na uhusiano na muktadha wa kisiasa uliopo.
Polisi wa Uswidi wamesajili tukio hili kama “uhalifu unaochochewa na chuki,” lakini uzoefu wa miaka ya karibuni umeibua mashaka makubwa kuhusu ufanisi wa hatua za kisheria. Waislamu wa Uswidi mara kadhaa wameonya kuwa kulegezwa kwa mifumo ya kisheria dhidi ya uchochezi wa chuki, kwa vitendo kunadhoofisha usalama wao.
Tukio hili linakuja katika mwendelezo wa msururu wa vitendo vya kudhalilisha Qur’ani Tukufu nchini Uswidi; vitendo ambavyo ndani yake watu na makundi yenye misimamo mikali, kwa uungwaji mkono wa polisi na chini ya mwavuli wa “uhuru wa kujieleza,” wamefanya vitendo vya kuchoma au kuitukana Qur’ani. Mwenendo huu umeifanya Uswidi kuwa moja ya vituo vikuu vya Uislamu-hofu barani Ulaya.
Mwaka 2022, vitendo vya uchochezi vya “Rasmus Paludan,” mwenye msimamo mkali mwenye uraia wa Denmark na Uswidi na kiongozi wa chama cha kupinga wahamiaji cha Stram Kurs, vilisababisha machafuko makubwa katika miji kadhaa. Ingawa baadaye alihukumiwa kwa kosa la kuchochea dhidi ya kundi la kikabila, shughuli zake zilichangia pakubwa kuhalalisha na kuzoesha chuki dhidi ya Waislamu.

Rasmus Paludan
Ripoti hiyo pia inaashiria nafasi ya watu kama “Salwan Momika,” raia wa Iraq anayeishi Uswidi, ambaye mwaka 2023 alichoma Qur’ani mbele ya Msikiti Mkuu wa Stockholm na kusababisha hasira kubwa katika nchi za Kiislamu pamoja na mvutano wa kidiplomasia; kitendo ambacho licha ya athari zake za kimataifa, kilifanyika kwa kibali rasmi cha polisi.
Mwenendo huu hauishii Ulaya pekee. Nchini Marekani pia, watu kama “Jake Lang,” mwanaharakati mwenye msimamo mkali na mgombea wa chama cha Republican kwa Seneti, kwa kufanya vitendo vya kudhalilisha Qur’ani katika mji wa Dearborn, jimbo la Michigan, na baadaye Plano, jimbo la Texas, wameonesha kuwa chuki dhidi ya Uislamu ni sehemu ya vita vikubwa vya kitamaduni vinavyoungwa mkono na mikondo ya mrengo wa kulia uliokithiri, Kizayuni na wapinga Uislamu; vita ambavyo vinatishia usalama wa Waislamu kote Magharibi.

Chapisho lenye chuki dhidi ya Uislamu la Jake Lang
Your Comment