Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kukamatwa kwa Rais wa Venezuela Nicolás Maduro na mkewe katika operesheni ya kijeshi iliyoendeshwa ndani ya Venezuela, akisema ilifanyika katika eneo lenye ulinzi mkali bila kupoteza maisha ya wanajeshi wa Marekani. Trump amesema alizungumza na Maduro wiki moja kabla ya operesheni hiyo na kumtaka asalimu amri, lakini hatua ya kijeshi ilichukuliwa baada ya mazungumzo kushindikana.

Kwa mujibu wa Trump, wawili hao wamesafirishwa hadi New York kukabiliana na mashtaka ya jinai, yakiwemo tuhuma zinazohusiana na vifo vya raia. Ameeleza pia kuwa Marekani itaendelea kuhusika katika mustakabali wa Venezuela, hususan katika sekta ya mafuta, huku akisisitiza kuwa uchaguzi uliomrudisha Maduro madarakani haukuwa wa haki.

Trump amesema operesheni hiyo ni ujumbe wa wazi kwa dunia kwamba Marekani haitavumilia vitisho, na inalenga pia kupambana na biashara ya dawa za kulevya inayodaiwa kusababisha vifo vya maelfu ya Wamarekani kila mwaka.

Your Comment