Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) –ABNA–, Waziri wa Viwanda, Madini na Biashara wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mohammad Atabak, amesema Iran ina dhamira ya kuimarisha zaidi ushirikiano wa kiuchumi na nchi wanachama wa Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia (EAEU), kwa lengo la kukuza biashara, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kufanikisha maendeleo ya pamoja.
Atabak aliyasema hayo alipokuwa akisoma ujumbe wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran, Mohammad Reza Aref, katika kikao cha pili cha Baraza la Serikali la Kimataifa la Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia kilichofanyika Ijumaa mjini Cholpon-Ata, Kyrgyzstan.
Katika ujumbe huo, Iran ilisisitiza umuhimu wa kutekeleza kikamilifu makubaliano ya biashara huria kati yake na Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia, kuendeleza njia za kimkakati za usafirishaji wa bidhaa, kuimarisha ushirikiano wa kifedha na kibenki, pamoja na kutumia ipasavyo uwezo wa pamoja wa kiuchumi ili kuchochea ukuaji wa uchumi na ustawi wa kikanda.
Aidha, Atabak alieleza kuwa katika miezi ya hivi karibuni Iran imekabiliwa na mashambulizi yaliyotekelezwa na Israel na Marekani. Alisema mashambulizi hayo yalisababisha vifo vya viongozi wa juu, maafisa wa kisiasa na kijeshi pamoja na maelfu ya raia.
Aliongeza kuwa miongoni mwa waliouawa walikuwemo wanafunzi 168 wa Shule ya Minab kusini mwa Iran, akielezea tukio hilo kuwa ni mauaji ya kikatili dhidi ya raia wasio na hatia.
Kwa mujibu wa ujumbe huo, Iran imeeleza kuwa pamoja na changamoto hizo za kiusalama, itaendelea kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na washirika wake wa kikanda ili kuchangia maendeleo, biashara na ustawi wa mataifa ya Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia.
Maoni yako