New York Times limechunguza madai kadhaa ya uwongo au yaliyotiwa chumvi aliyotoa Rais wa Marekani Donald Trump wakati wa hotuba yake katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hapo jana na kueleza kwamba, wakati Trump amedai kuwa Marekani na Venezuela zinamiliki zaidi ya 60% ya mafuta duniani, data zilizochapishwa na Idara ya Taarifa za Nishati ya Marekani zinaonyesha kwamba nchi hizo mbili kwa pamoja zinamiliki 22% ya akiba ya mafuta duniani, au mapipa bilioni 349. Uzalishaji wao pia unachangia 23% ya uzalishaji wa kimataifa, si 60%.
Katika hotuba yake hiyo, Trump alidai pia kwamba amehitimisha vita vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Ukanda wa Ghaza na kuokoa maisha ya maelfu! Hii ni licha ya ukweli kwamba, kwa mujibu wa New York Times, usitishaji mapigano uliofikiwa Oktoba 2025 haukukomesha kikamilifu mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Israel dhidi ya Ukanda wa Ghaza, na tangu wakati huo, zaidi ya Wapalestina elfu moja wamepoteza maisha katika Ukanda huo.
Na hii ni pamoja na kwamba, waziri mkuu wa utawala wa kizayuni Benjamin Netanyahu ametangaza hadharani kupinga mpango wa vipengele 15 uliopendekezwa na serikali ya Trump kuhusiana na Ghaza.
Katika uga wa vita vya kupambana na madawa ya kulevya, Trump amedai katika hotuba yake mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kwamba mashambulizi ya Marekani dhidi ya boti za magendo ya dawa za kulevya yamekomesha 97% ya usafirishaji wake kimagendo kwa njia ya baharini na kwamba biashara ya mihadarati imepungua kwa kiasi hicho hicho. Hata hivyo gazeti la New York Times lilmeripoti kuwa dai hilo pia halina mashiko wala msingi wowote, kwa sababu kwa mujibu wa wataalamu katika eneo, mashambulizi hayo yamepelekea kubadilika njia tu za kufanyia magendo. Ripoti ya ndani ya Idara ya Kupambana na Madawa ya Kulevya nayo pia inaonyesha kuwa, mashambulizi hayo hayajaathiri mnyororo wa usafirishaji wa kokeini au bei yake ndani ya Marekani.
Katika hotuba yake, Trump ametia chumvi pia kuhusu kuwepo kwa wingi mno akiba ya risasi, silaha na zana za kivita, licha ya kiwango kikubwa cha zana hizo kutumika wakati wa vita dhidi ya Iran, sambamba na kudai kwamba amefanya kazi ya kuhitimisha vita vinane. Kwa mujibu wa New York Times, baadhi ya vita hivyo vimeishia kwenye hatua ya usitishaji mapigano tu wakati vingine havijamalizika moja kwa moja.
Kwa kumalizia New York Times limesisitiza kwamba takwimu zilizotangazwa katika hotuba ya Trump haziungwi mkono na ripoti na data zilizotolewa hadharani, hususan katika uga wa mafuta, madawa ya kulevya, akiba ya silaha na vita…/
Maoni yako