Ayatullah Sayyd Ali Khamenei alisisitiza kuwa, kama umma wa Kiislamu katika nchi mbali mbali duniani utashikamana na kijihadi, na kusimama imara na kuwa na dhina nzuri juu ya msaada wa Mwenyezi Mungu, basi bila ya shaka ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kuwanusuru na kunusuru dini yake.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesisitiza kwamba matukio ya mwaka mmoja uliopita katika eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika ni katika bishara njema na ni katika neema na rehema za Mwenyezi Mungu na kuongeza kuwa, matukio hayo yanapaswa kuhesabiwa kuwa ndio kwanza na ndio mwanzo wa uwezo wa Mwenyezi Mungu na kusubiri ushindi mwingine mkubwa utakaopatikana katika njia hiyo. Ayatullah Khamenei Kiendelea kusema kuwa, kupigana jitihada bila mchoko ni kuipa jihadi haki yake, ni lazima kuweza kupatikana nusra na ushindi wa Mwenyezi Mungu na kuongeza kuwa: Jamuhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi chote cha miaka 32 iliyopita, imekuwa ikikabiliwa na mashinikizo kutoka kwa maadui lakini kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu imefanikiwa kushinda, na itaendelea na njia yake hiyo kwa nguvu za Mwenyezi Mungu.
Pia amegusia suala la Syria na kusema: Kama suala la Syria litaangaliwa kwa mtazamo mpana basi njama za Marekani na mkono wa dola hilo utaonekana waziwazi na ni jambo la kusikitisha kuona kuwa baadhi ya nchi za nje na za eneo hili zinashirikiana na Marekani katika njama hizo. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislam amesisitiza kuwa, lengo kuu la njama hizo za Marekani nchini Syria ni kutoa pigo kwa harakati ya muqawama katika eneo hili na sababu ni kuwa Syria inaunga mkono mapambano na muqawama wa Palestina na ule wa Lebanon.Ameongeza kuwa, Wamarekani na baadhi ya nchi za Magharibi wanataka kulipiza kisasi kutokana na kufeli vibaya siasa zao hivi karibuni katika eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika ikiwa ni pamoja na nchini Misri na Tunisia na ndio maana wameamua kumalizia hasira zao nchini Syria.Amebainisha wazi kwamba msimamo wa Jamuhuri ya Kiislam ya Iran kuhusiana na Syria ni kuunga mkono marekebisho yoyote yale yenye manufaa kwa wananchi wa nchi hiyo, na kupinga uingiliaji wa Marekani na nchi vibaraka wake katika masuala ya ndani ya Syria.Aidha huku akiashiria matamshi ya wanachama wa chama cha Jihadul Islami cha Palestina kuhusiana na maendeleo makubwa na ya kustaajabisha ya kisayansi ya Iran, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, harakati za kielimu nchini Iran ni pana na zimeenea katika kada na sekta zote za kielimu na kiteknolojia na baadhi ya wakati inakuwa vigumu kwa watu wengi hata kutasawari na kufikiria maendeleo hayo.Ayatullah Khamenei ameelezea matumaini yake kuwa, harakati hizo za kielimu zitashuhudiwa pia katika nchi nyingine za Kiislamu kama vile Misri, Tunisia na Libya na hatimaye umma wa Kiislam utaweza kuwa na nguvu kubwa za kielimu na kiteknolojia. Kwa upande wake, Dk. Ramadhan Abdullah, Katibu Mkuu wa chama cha Jihadul Islam cha Palestina sambamba na kutoa mkono wa pongeza kwa mnasaba wa siku za Alfajiri Kumi za maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislam ya Iran, ametoa ripoti kuhusu matukio ya Palestina hasa ya Ukanda wa Ghaza na kusema kuwa, mwamko wa Kiislamu na matukio yanayoendelea kushuhudiwa katika eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika ni fursa nzuri sana kwa ajili ya mataifa ya Waislamu hasa wanancihi wa Palestina na kwamba kila mtu anapaswa kuwa macho mbele ya fitna na njama za maadui wenye nia ya kuvuruga matukio hayo.Ameongeza kuwa, ustaarabu wa Kiislam kwa mara nyingine umeanza kurejea kwenye kipindi chake cha ustawi wa hali ya juu na kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina nafasi muhimu mno na isiyo na mbadala katika kustawi huko ustaarabu wa Kiislamu na ni kwa sababu hiyo ndio maana kambi ya mabeberu ikawa inalishinikiza kupindukia taifa la Iran.Katibu Mkuu wa Jihadul Islam ya Palestina aidha ameashiria matukio ya Syria na kusema kuwa, Wamagharibi wanafanya njama za kuitoa Syria katika kambi ya muqawama kutokana na kuwa nchi hiyo ni moja ya kambi kuu za muqawama katika eneo hili.Naye Dk. Muhammad, mmoja wa viongozi wa Jihadul Islami ya Palestina ametoa ripoti kuhusu hali ya hivi sasa ya Ukanda wa Ghaza huko Palestina na huku akiashiria maendeleo makubwa ya kielimu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema kuwa, maendeleo hayo ya kustaajabisha ni fakhari kwa Waislamu wote duniani.