Saeed Jalili, ambaye pia ni mkuu wa baraza la usalama la Iran, aliwasili Syria mapema Jumanne, akitokea Beirut, mji mkuu wa Lebanon. Huko alikuwa na mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo. Iran, ambayo ni mshirika mkuu wa Syria, imekuwa ikikosoa ushirikiano unaotolewa na nchi kama Marekani, Uturuki, Saudi Arabia na Qatar kwa waasi wanaopamabana na vikosi vya Assad. Mbali na hayo, Iran ina wasiwasi juu ya hatma ya raia 48 wa nchi hiyo, waliotekwa na waasi mwishoni mwa wiki iliyopita.
aziri wa mambo ya nje wa Iran, Ali Akbar Salehi, atafanya ziara nchini Uturuki Jumanne kufanya mazungumzo juu ya mzozo wa Syria na juu ya kisa cha raia hao 48 wa Iran waliotekwa. Mwanadiplomasia mmoja wa Uturuki amelieleza shirika la habari la AFP kwamba Salehi atakutana na mwenzake wa Uturuki, Ahmet Davutoglu na watajadili zaidi kuhusu mzozo wa Syria.
Nchini Syria kwenyewe, mapigano yanaripotiwa kuendelea katika mji wa Aleppo uliopo kaskazini mwa nchi hiyo. Majeshi ya serikali leo yameendelea na juhudi zake za kuteka maeneo ambayo sasa yanakaliwa na waasi. Wapigananaji wasiopungua 25 wameuwawa katika machafuko yaliyotokea leo. Mauaji hayo yalitokea baada ya waasi kukishambulia kituo cha kuzalisha umeme na hivyo, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya taifa, kuwalazimisha wanajeshi wa serikali kuwashambulia waasi na kuuwa 25 kati yao.