28 Oktoba 2012 - 10:45

Watu 20 wameuawa na wengine 11 kujeruhiwa katika mashambulizi ya mabomu nchini Syria licha ya mapatano ya kusitisha mapigano ili kuwaruhusu wasyria kusherehekea sikukuu ya Eid al-Adha.

Mashambulizi hayo yalitokea jana muda mfupi tu baada ya jeshi la Syria kutoa taarifa ikisema vurugu zilishuhudiwa kote nchini Syria jana asubuhi. Watu 20 waliuawa wakiwemo watoto baada ya magari mawili yaliyokuwa yametegwa mabomu kulipuka kwa nyakati tofauti katika miji ya Damascus na Daraa.

Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi, awali makundi yenye silaha yalishambulia kituo cha ukaguzi cha kijeshi kusini mwa mkoa wa Daraa na kuvamia maeneo manne ya kijeshi katika mkoa wa kaskazini wa Idlib. Taarifa hiyo pia imesema mapatano ya kusimamisha mapambano pia yalivunjwa katika mkoa ya mashariki wa Deir al-Zour, mkoa wa Homs na vitongoji vya mji mkuu wa Damascus. Taarifa hiyo imeeleza kuwa jeshi la Syria lililazimika kujibu mashambulizi ya waasi hao.