Taarifa iliyotolewa na ikulu ya nchi hiyo imesema, rais Zuma alimtembelea Mandela jana jioni na kumkuta kiongozi huyo akiwa bado katika hali mbaya, hivyo kumfanya kiongozi huyo kufuta ziara aliyokuwa aifanye Msumbiji. Akiwa nchini humo, rais Zuma pia alitarajia kuhudhuria mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC, unaohusu uwekezaji kwenye sekta ya miundombinu katika kanda hiyo.
Rais Zuma ametoa shukrani kwa niaba ya serikali yake kwa wananchi wa Afrika Kusini ambao wanaendelea kumwombea Mandela.
Hali ya usalama imeongezwa katika hospitali alipolazwa kiongozi huyo, na polisi wanaosimamia mageti ya hospitali hiyo wanatumia vifaa maalum kukagua magari kabla hayajaruhusiwa kuingia hospitalini hapo.
Mandela alilazwa kwenye hospitali ya Medi Clinic Heart iliyoko Pretoria kutokana na maambukizi ya homa ya mapafu.