Serikali ya Marekani itatuma wanajeshi zaidi katika kutekeleza kampeni yake dhidi ya kundi magaidi wa Daesh, huku jitihada za kimataifa dhidi ya kundi hilo zikiendelea. Ufaransa imesema vijana wengi, wakiwemo raia wake wanajiunga na kundi hilo la kigaidi.
Marekani inapanga kuwatuma wanajeshi wengine 1,500 kwenda kutoa mafunzo na ushauri kwa wanajeshi wa Iraq katika vita dhidi ya magaidi wa Daesh. Wizara ya ulinzi imesema wanajeshi hao wapya watapelekwa Iraq katika wiki chache zijazo bila kusubiri idhini ya bunge ya kuufadhili ujumbe huo.
Maafisa awali walidokeza kuwa waliwahitaji wabunge kuidhinisha ufadhili kabla ya wizara ya ulinzi kuanzisha operesheni hiyo, lakini Jenerali Lloyd Austin, mkuu wa majeshi ya Marekani katika Mashariki ya Kati, akapendekeza kuanzisha mpango huo kwa kutumia raslimali ambazo tayari anazo.
Makamu wa Rais Joe Biden leo atakuwa kiongozi wa karibuni kabisa wa Marekani wanaojaribu kuishinikiza Uturuki kuchukua jukumu lake katika kampeni ya muungano wa kimataifa dhidi ya magaidi wa Daesh. Ziara ya Biden inakuja baada ya wiki kadhaa za majibizano ya hadharani baina ya washirika hao wawili wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO.
Rais wa Uturuki anasisitiza kuwa kama Marekani inataka msaada wake, lazima izingatie zaidi namna ya kumwondoa madarakani rais wa Syria Bashar al-Assad na wala siyo kupambana na magaidi wa Daesh tu. Recip Tayyip Erdogan anataka pawekwe eneo la usalama la kijeshi kaskazini mwa Syria ili kuwapa wapiganaji wa msimamo wa wastani nafasi ya kujiimarisha na kufanya mashambulizi dhidi ya Assad. Nayo Marekani inasisitiza kuwa haitaki kuingia vitani dhidi ya Assad ikisema haiwezekani kuwekwa amri ya kutoruka ndege dhidi ya jeshi la Syria. Kwingineko, Rais wa Syria Bashar al-Assad amesema “ushirikiano wa kimataifa” unahitajika ili kuliangamiza magaidi wa Daesh. Assad amesema kanda nzima inakabiliwa na kitisho cha wapiganaji hao wa jihadi ambao anahoji kuwa waliibuka kutokana na matunda ya sera mbovu na za uchokozi zilizowekwa na wale walioanzisha vita dhidi ya Syria.
Katika hatua nyingine Iraq na Uturuki zimekubaliana kuwa na ushirikiano wa karibu wa usalama na ujasusi kutokana na kitisho kilichopo kutoka kwa magaidi wa Daesh. Davutoglu amepinga madai kuwa nchi yake iliwezesha kusafirishwa kwa wanamgambo kupitia mipaka yake na kuingia nchini Syria. Alisema Uturuki hupokea watalii milioni 35 kila mwaka na haiwezi kuwazuia watu kuingia nchini humo, isipokuwa kama wana kesi dhidi yao.
Mjini Paris, ofisi ya mwendesha mashtaka imesema wapelelezi wameanzisha rasmi uchunguzi wa ugaidi dhidi ya raia watatu wa Ufaransa ambao wameonekana wakifanya jinai dhidi ya wananchi wasio na hatia ambao walitoa wito kupitia video ya propaganda ya kufanywa mashambulizi nchini Ufaransa. Watu hao watatu wanatoa wito kwa Wafaransa kuungana nao vitani au wafanye mashambulizi ndani ya nchi yao.
Yafaa kuashiria kuwa, Uturuki inakosa amani baada ya kuona majeshi ya Syria yanazidi kusonga mbele na kuwaangamiza magaidi wanaohatarisha serikali ya Bashar asad, kwani Uturuki inahesabika kuwa ndiyo msada mkubwa wa magaidi hao, hivyo ushindi wa Bashar Asad, utapelekea hali ya Uturuki kuwa matatani, ndio maana nchi hiyo inasisitiza kuondolewa madarakani rais wa Syria ambaye amechaguliwa na wananchi kwa demokrasia.