Serikali ya Jamhuri ya kiislamu ya Iran inasema ushahidi uliopelekwa Umoja wa Mataifa juu ya mpango wake wa nyuklia ni wa kubuni na wenye makosa kadhaa wa kadhaa.
Katika taarifa yake kwa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki, IAEA, Jamhuri ya kiislamu ya Iran imekanusha tuhuma kwamba imekuwa ikilizuia shirika hilo kufanya uchunguzi wake, hatua ambayo imechukuliwa na IAEA kuwa ni ushahidi tosha kuwa Iran ina mpango wa kutumia programu kutengeneza makombora ya nyuklia.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Iran, Jamhuri ya kiislamu ya Iran imekuwa ikiipa IAEA ushirikiano wa kutosha.
Mazungumzo ya kufikia makubaliano ya mwisho kati ya Iran na mataifa sita yenye nguvu duniani, yalirefushwa hadi mwakani baada ya mazungumzo ya mwezi uliopita mjini Vienna, Austria kushindwa kumalizika na mkataba wa makubaliano. Mapema mwezi Novemba, IAEA ilitoa taarifa inayoishutumu Iran kwa kutoa ushahidi unaokanusha wasiwasi wa jumuiya ya kimataifa kuhusu vinu vyake vya nyuklia.
Mzozo wa nyuklia ya Iran umeleta mvutano mkubwa kati ya nchi hiyo na nchi za magharibi kwa zaidi ya miaka 10, ambapo nchi za magharibi zinasadiki kuwa Jamhuri ya kiislamu ya Iran inampango wa kutengeneza makombora ya nyuklia, na kwa upande wa Iran inapinga madai hayo na kusema kuwa inamalengo ya amani na kwamba haina haja ya makombora ya maangamizi kwani ni haramu kwa mujibu wa itikadi za kiislamu.