Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, amesema nchi yake iko tayari kufanya kila iwezalo, ili pande hasimu nchini Ukraine zikae kitako kutafuta suluhisho la mzozo wao. Akizungumza kwa njia ya simu na mwenzake wa Marekani, John Kerry, mapema leo, Lavrov amesema hakuna njia yoyote ya kupatikana kwa amani, bila ya serikali kuu ya Ukraine mjini Kiev, kuzungumza moja kwa moja na wawakilishi wa makundi ya waasi wanaopigania kujitenga kwa maeneo ya kusini mashariki mwa nchi hiyo. Lavrov ameituhumu Ukraine kwa kuamua njia za kijeshi badala ya mazungumzo kumaliza mizozo kati yake na waasi hao. Kwenye mazungumzo hayo, Kerry alipendekeza kuongezwa kwa washiriki kwenye kundi la wapatanishi wa kimataifa wa mzozo huo, ili kusaidia mazungumzo kati ya serikali ya Ukraine na viongozi wa mikoa ya Donestk na Luhansk, wanaopigania kujitenga. Lavrov amefanya mazungumzo kama hayo na mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya.
Wakati huo huo Rais Petro Poroshenko wa Ukraine anasema mawasiliano yanathibitisha kwamba waasi wanaotaka kujitenga kusini mashariki mwa nchi yake, wanahusika na mashambulizi ya roketi dhidi ya basi moja la abiria, yaliouwa watu 30 huko Mariupol. Akikutana na Baraza lake la Usalama hivi leo, Poroshenko amesema mawasiliano hayo kwa njia ya simu yanatoa ushahidi usio shaka kuwa waasi hao wanaosaidiwa na Urusi ndio waliofanya mashambulizi hayo. Awali, kiongozi wa waasi hao, Alexander Zakharchenko, alikuwa ametangaza kuwa vikosi vyake vingelifanya operesheni mjini Mariupol, lakini amekanusha kuhusika na mashambulizi hayo ya jana. Wafanyakazi wa huduma za dharura waliokota vipande vya maroketi yaliyotumika kwenye mashambulizi hayo, kwa ajili ya uchunguzi. Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa limetoa msaada wa mablanketi kwa watu waliopoteza makaazi yao kwenye mashambulizi hayo.