Waandamanaji wanane wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa na vikosi vya usalama, wakati wakishiriki maandamano ya kuadhimisha miaka minne ya vuguvugu la umma, lililomuondoa madarakani Rais Hosni Mubarak. Kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha al-Jazeera, watu wengine watatu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo, wameuawa nje ya mji mkuu wa Misri, Cairo. Wawili kati ya watu hao waliuliwa kwenye jimbo la Beheira, ambapo polisi inadai walikuwa wakitega bomu. Mwengine wa tatu aliuawa wakati akitupiana risasi na polisi kwenye mji wa Alexandria. Ulinzi umeimarishwa kwenye miji kadhaa mikubwa nchini humo hivi leo, kukihofiwa machafuko katika maadhimisho hayo. Hapo jana, mwanamke mmoja alipigwa risasi na kuuawa wakati akishiriki maandamano ya kuwakumbuka waandamanaji 900 waliouawa kwenye vuguvugu hilo la mwaka 2011. Wapinzani wa utawala wa Rais Abdel-Fattah el-Sissi, wameapa kumiminika mitaani hivi leo kuadhimisha kile wanachokiiita mapinduzi ya umma yaliyotekwa nyara na jeshi.