Mfalme Abdullah wa Pili wa Jordan ameahidi nchi yake itachukua hatua kali dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh, kutokana na mauaji ya rubani wake Muath al-Kasaesbeh, yaliyofanywa na kundi hilo.
Kauli hiyo ameitoa wakati ambapo Marekani imeeleza wazi kwamba iko pamoja na Jordan katika kuwaangamiza magaidi wa kundi la Daesh. Akizungumza na makamanda wa juu wa jeshi na maafisa wa usalama mjini Amman, Mfalme Abdullah, ameapa kuwa Jordan itaendesha mapambano makali yasiyo na huruma dhidi ya magaidi wa kundi Daesh, kwa sababu damu ya shahidi huyo haitapotea bure. Kasaesbeh, mwenye umri wa miaka 26, aliuawa na Daesh kwa kuchomwa moto akiwa hai katika kizimba.
Ameahidi mapambano na IS licha ya Jordan kuwanyonga wanamgambo wawili wa Iraq, akiwemo mfungwa wa kike mwenye msimamo mkali, Sajida al-Rishawi, ambaye wapiganaji wa Daesh walitaka aachiwe huru ili kubadilishana na mateka huyo wa Jordan.
Kauli hiyo ya Mfalme Abdullah ameitoa baada ya mkanda wa video kuwekwa kwenye mtandao ukimuonyesha Kasaesbeh akichomwa moto.
Kutokana na mauaji hayo, Mfalme Abdullah alikatisha ziara yake nchini Marekani na kurejea nyumbani kulihutubia taifa, ambako kumefanyika maandamano ya kutoa wito wa nchi hiyo kulipiza kisasi na hivyo kuondoa wasiwasi uliokuwepo awali wa kupambana na na kundi hilo la Daesh.
Wakati huo huo, Rais Barack Obama wa Marekani, nchi ambayo ni mshirika mkuu wa Jordan ameeleza wazi kwamba yuko pamoja na nchi hiyo kuliangamiza kundi la kigaidi la Daesh. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Jen Psaki, amesema Marekani iko pamoja na watu wa Jordan.
Psaki alisema, ''Serikali ya Jordan ni mshirika muhimu. Haya yalikuwa mauaji mabaya dhidi ya raia wa Jordan, ambayo yataifanya jumuiya ya kimataifa kujizatiti zaidi katika kuiangamiza Daesh. Katika suala la kuchukua hatua, bila shaka tunafahamu kuhusu adhabu ya kifo, iliyotekelezwa.''
Marekani inapanga kuisaidia nchi hiyo kwa kuipatia silaha za kupambana na Daesh. Seneta Joe Manchin, amesema Jordan inapaswa kupewa vifaa vyote muhimu vya kijeshi. Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Kijeshi ya Baraza la Seneti la Marekani, Senata John McCain amesema anatarajia baraza hilo litaiidhinisha kirahisi sheria hiyo inayofaa. Aidha, ameikosoa sera ya serikali ya Rais Obama ya kupambana na Daesh, akisema haina mkakati kabisa.
Ama kwa upande mwingine maafisa wa usalama wa Marekani wamesema Umoja wa Falme za Kiarabu-UAE, umesema utaacha kufanya mashambulizi ya anga dhidi ya wanamgambo wa Daesh nchini Syria, yanayoongozwa na Marekani. Maafisa hao wamesema umoja huo utaacha kushiriki kwenye kampeni hiyo ya anga baada ya ndege ya kivita ya Jordan kuanguka nchini Syria wakati wa operesheni mwezi Disemba na rubani wake kuuawa na kundi la kigaidi la Daesh.
Wakati hayo yanaendelea wito umetolewa kwa Uingereza kuongeza nguvu za kupambana na magaidi wa Daesh
Kamati ya kuteuliwa ya maswala ya Ulinzi ndani ya Bunge hilo imesema Uingereza imeshiriki asilimia 6 tu ya mashambulizi ya anga dhidi ya kundi hilo la Jihad na kusema kuwa wanashangazwa kwa kuwa haifanyi jitihada za hali ya juu.
Wabunge wamesema Wanamgambo hawa wamejiimarisha sehemu za nchi ya Iraq na Syria .
Daesh imekuwa ikishikilia maeneo mengi na imekuwa ikijihusisha na vitendo vya kikatili ikiwemo kukata vichwa vya Mateka Raia wa Uingereza.
Ripoti inasema kuwa Daesh kujitokeza kutoka eneo la Mashariki ya kati ni tishio kwa usalama wa Dunia.
Serikali ya Uingereza imelaumiwa kwa kutokuwa na mbinu za kijeshi.
Ndege za kijeshi zilianza kupeleka Wanajeshi wake nchini Iraq mwezi Septemba baada ya Wabunge kuunga mkono Operesheni za kijeshi dhidi ya magaidi wa Daesh nchini Iraq.
Hata hivyo, Bunge halikuombwa kupiga kura kuunga mkono mpango wa Operesheni za kijeshi dhidi ya Daesh nchini Syria.
Kamati ilifanya ziara nchini Iraq Mwezi Desemba na kubaini kuwa kulikuwa na Wanajeshi watatu pekee nje ya Miji ya kikurdi, ikilinganishwa na Wanajeshi 400 wa Australia, 280 wa Italia na 300 wa Uhispania.
Ripoti hiyo imeitaka Serikali ya Uingereza kufanya tathimini ya hali ilivyo nchini Iraq kisha kutoa msaada kwa vikosi vya usalama vya Iraq na Wapiganaji wa Peshmerga watakapokuwa tayari kwa mapigano dhidi ya Daesh.