Rais Vladimir Putin wa Urusi amefanya ziara nchini Hungary ambapo amekutana na waziri mkuu Viktor Orban kuzungumzia masuala ya nishati. Asilimia 60 ya gesi inayotumika Hungary inatokea Urusi na Urusi vile vile ina mpango wa kujenga vinu viwili vya nyuklia nchini Hungary. Kabla ya Putin kuwasili, watu wapatao 2,000 waliandamana mjini Budapest kupinga ujio wa rais huyo wa Urusi. Wachambuzi wanasema Putin ameitumia ziara yake ya siku moja kuuonyesha ulimwengu kuwa bado ana rafiki barani Ulaya, yaani Viktor Orban. Nchi nyingi za Magharibi zinamshutumu Putin kutuma wanajeshi kuwaunga mkono waasi Mashariki mwa Ukraine. Akiwa Hungary Putin alizungumzia pia mzozo huo wa Ukraine ambapo ametaka wanajeshi wa serikali wasizuiliwe kuweka silaha zao chini ili amani irejee.
Na hukuko Ugiriki, waziri wa fedha wa nchi hiyo Yanis Varoufakis, amesema atauomba Umoja wa Ulaya urefushe mpango wa uokozi kwa ajili ya nchi yake. Akizungumza na kituo kimoja cha televisheni cha hapa Ujerumani Varoufakis amesema anataka mpango huo, ambao muda wake ulikua uishe mwishoni mwa mwezi huu, urefushwe kwa miezi kadhaa, kuipa muda Ugiriki kuandaa mpango mpya. Serikali ya Ugiriki itatuma barua kwa mkuu wa kundi la mawaziri wa fedha wa nchi zinazotumia sarafu ya Euro, Jeroen Dijsselbloem, kuomba mpango urefushwe kwa miezi sita. Hayo yanakuja baada ya Varoufakis kushindwa kufikia makubaliano na wenzake wa Umoja wa Ulaya katika mkutano uliofanyika Brussels Jumatatu. Waziri wa fedha wa Ujerumani, Wolfgang Schäuble, ameikosoa Ugiriki, akisema nchi hiyo inataka kuongezewa fedha bila kusema ina mipango gani ya kubana matumizi na kurejesha mkopo wa Euro bilioni 240 uliotolewa na Umoja wa Ulaya.