Rais wa Marekani Barack Obama amewakosoa vikali wanasiasa wa chama cha Republican kuhusiana na barua waliowaandikia viongozi wa jamhuri ya kiislamu ya Iran iliyoonya kwamba mkataba wowote na Marekani kuhusu mpango wake wa nyuklia huenda ukafutwa na rais mpya wa Marekani atakayechaguliwa. Maseneta 47 wa chama cha Republican, wakiwemo wanaotarajiwa kugombea urais wa Marekani mwaka ujao, walichukua hatua hiyo ya kuwasiliana moja kwa moja na viongozi wa jamhuri ya kiislamu ya Iran katika juhudi za kuyasambaratisha mazungumzo muhimu yanayolenga kutafuta makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wenye utata.
Makamu wa rais wa Marekni Joe Biden amewakosoa maseneta hao kwa kuzihujumu juhudi za kidplomasia akisema wanaiweka Marekani katika hatari ya kutoaminika. Waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Iran Mohammed Javad Zarif ameipuzilia mbali barua hiyo akiita njama ya propaganda.