Ufaransa imeshambulia maeneo ya wapiganaji wa kundi la kigaidi la Daesh katika eneo la Tikrit nchini Iraq kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa mashambulio ya kimataifa dhidi ya wanamgambo hao wa kundi la kigaidi.
Msemaji wa serikali ya Ufaransa hakutoa maelezo zaidi ya iwapo ndege za kijeshi ama ndege zisizokuwa na rubani zilitumika kufanya mashambulio hayo, na amekataa kutoa maelezo zaidi kuhusu maeneo yaliyoshambuliwa.
Majeshi ya Marekani yametangaza hapo kabla kufanya mashambulizi ya anga dhidi ya maeneo ya kundi la kigaidi la Daesh mjini Tikrit pamoja na majeshi ya muungano baada ya kumuomba waziri mkuu wa Iraq Haider al-Abadi awaruhusu kufanya mashambulizi hayo.
Maelfu ya wanajeshi wa Iraq , maafisa wa polisi na jeshi la anga wamewekwa ili kuukamata mji wa Tikrit , ambao wapiganaji wa kundi la kigaidi la Daesh wanajitahidi kuulinda kwa kutega mabomu mitaani pamoja na majengo mbali mbali ndani ya mji huo.
Ushindi wa majeshi ya Iraq katika mapambano hayo unatokana na msaada wa pekee kutoka kwa Jeshi la Quds la Iran likiongozwa na Meja Jeneral Qassim Suleiman.