Bunge la Uturuki limepitisha sheria kuhusu usalama wa ndani, ambayo imepunguzwa makali ikilinganishwa na ya awali iliyozusha utata na kulaaniwa na vyama vya upinzani. Sheria hiyo imepitisha leo asubuhi baada ya majadiliano usiku kucha katika bunge ambalo linadhibitiwa na chama Haki na Maendeleo, AKP.
Shirika la habari la Dogan limesema kuwa kati ya wabunge 231 walioshiriki. 199 walipiga kura kuikubali sheria hiyo, huku 32 wakipiga zao kuipinga. Upinzani ulikuwa umeupinga vikali mswada wa kwanza wa sheria hiyo, ukisema ingempa mamlaka rais Recep Tayyip Erdogan kuifanya Uturuki nchi inayotawaliwa ki-polisi, akiwa na uwezo wa kukandamiza upinzani.
Katika kutafuta muafaka, serikali ilikuwa imependekeza mswada uliopunguzwa makali ili uweze kupitishwa na bunge. Vipengele 69 vya sheria hiyo vimepitishwa, lakini vingine 63 vimerudishwa katika kamati ya bunge ili vijadiliwe zaidi.