2 Aprili 2015 - 19:03
Israel yaanza kuwahamisha wahamiaji haramu

Benjamin Netanyahu amesema muafaka umepatikana na nchi mbili barani Afrika ambazo ni salama zitakazowapa hifadhi wahamiaji hao.

Israel imeanza kuwasafirisha waomba hifadhi kuwapeleka katika nchi ambako siyo makwao, wengi wakiwa Waeritrea walioingia nchini humo kinyume cha sheria. Waeritrea saba wanaoishi katika kituo kimoja cha jangwa la Negev nchini Israel wamepata barua zinazosema wana siku 30 kuondoka kuelekea nchi ambayo haikutajwa. Kama watakaidi amri hiyo, watakamatwa na kuzuiliwa. Jina la nchi ya tatu itakayowapa hifadhi halikutajwa katika taarifa ya kwanza kwa wahamiaji hao, lakini vyombo vya habari vya Israel vinasema nchi hizo ni Rwanda na Uganda. Waziri wa Mambo ya Ndani Gilad Erdan, wa chama cha siasa mrengo wa kulia cha Likud kinachoongozwa na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amesema muafaka umepatikana na nchi mbili barani Afrika ambazo ni salama zitakazowapa hifadhi wahamiaji hao.