Serikali ya Jamhuri ya kiislamu ya Iran imetaka kuazishwa haraka mazungumzo ya amani kati ya makundi yanayohasimiana nchini Yemen.
Shirika la habari la jamhuri ya kiislamu ya Iran IRNA, limetangaza leo kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammed Javad Zarif, ametoa wito huo wakati wa mazungumzo ya simu kati yake na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, jana. Wito huo umetolewa wakati ambapo wananchi na wanamapinduzi wa kishia wa Huthi wanaoungwa mkono na Iran wakipambana na vikosi vya magaidi wa Alqaida na Daesh vinavyosaidiwa na mashambulizi ya anga yanayoongozwa na Saudi Arabia.
Zarif aligusia mpango wenye vifungu vinne wa kumaliza mzozo wa Yemen, akisisitiza umuhimu wa mazungumzo kati ya wanamapinduzi wa kishia wa Huthi na vikosi vinavyomtii Rais Abed-Rabbo Mansour Hadi vikisaidiwa na magaidi wa Daesh na Alqaida, rais aliyekimbilia Saudi Arabia, na kwamba Iran iko tayari kusaidia kuutatua mzozo huo.
Wakati huo huo, rais wa zamani wa Yemen, Ali Abdullah Saleh amesema leo kuwa hatoondoka nchini humo na hivyo kupuuza taarifa za vyombo vya habari vya nchi za kiarabu za Ghuba kwamba anatafuta eneo salama la kukimbilia.