Ikulu ya Marekani ya White House imekiri kwamba mateka kutoka Marekani na Italia wameuwawa katika shambulio la ndege isiyokuwa na rubani katika viwanja vya majengo yanayowahifadhi wapiganaji wa al-Qaeda nchini Pakistan mwezi Januari. Muda mfupi baada ya tangazo kutolewa, rais Barack Obama alitumia mkutano na waandishi habari katika ikulu ya Marekani kuomba radhi kwa familia za wahanga. Amesema anachukua dhima ya operesheni yote ya kupambana na magaidi , ikiwa ni pamoja na hii, na kwamba ameamuru uchunguzi kamili wa tukio hilo. Wafanyakazi hao wawili wa mashirika ya kutoa misaada waliouwawa katika mashambulizi hayo ni Warren Weinstein , Mmarekani ambaye alikamatwa na al-Qaeda mwaka 2011, na Mtaliani Giovani Lo Porto, ambaye alikamatwa mwaka mmoja baadaye. Pia Mmarekani mwanachama wa kundi la al-Qaeda aliuwawa katika shambulio hilo.