(ABNA24.com) Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kwamba mpango unaojulikana kama Muamala wa Karne kamwe hautafanikiwa.
Akizungumza jana Jumatano asubuhi katika hotuba za swala ya Idul Fitr katika Muswala wa Imam Khomeini (MA) hapa mjini Tehran, yatullah Ali Khamenei ameashiria suala la Palestina na mpango wa hiana wa Marekani mashuhuri kama Muamala wa Karne na kusema kuwa hilo ndilo suala la kwanza linalopasa kupewa umuhimu katika ulimwengu wa Kiislamu. Amesema: Hiana inayofanywa na baadhi ya nchi za Kiislamu kama vile Bahrain na Saudi Arabia ndiyo imeandaa uwanja wa kuandaliwa mpango kama huo wa hiana.
Ameashiria uenyeji wa mkutano wa Muamala wa Karne unaofanywa na Bahrain na kusema: Mkutano huo umeandaliwa na Marekani na watawala wa Bahrain kukubali kuwa wenyeji wake kutokana na udhaifu wa roho pamoja na siasa zao zilizo dhidi ya wananachi na Uislamu na kutahadharisha kwamba watawala wa nchi hiyo na wa Saudia wanapasa kutambua ni kinamasi hatari cha aina gani wanachotembea ndani.
Mpango wa Maumala wa Karne ni mpango uliopangwa na kupendekezwa mara tu baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kuingia Ikulu ya White House, na kwa masikitiko makubwa, kuungwa mkono na baadhi ya tawala vibaraka za Kiarabu. Mpango huo unaotazamiwa kuzinduliwa rasmi katika kikao cha kiuchumi cha Manama tarehe 25 na 26 za mwezi huu wa Juni, utaanza kutekelezwa katika hali ambayo katika vikao vyao vya hivi karibuni huko mjini Makka, watawala wa nchi za Kiarabu walipuuzilia mbali na kukataa kujadili suala muhimu la Palestina, jambo ambalo linaanika wazi hiana na usaliti wao kwa malengo ya taifa la Palestina.
Rais wa Marekani sasa anatoa mashinikizo makubwa dhidi ya watawala wa Saudia Arabia, Bahrain na Imarati ili wagharamie utekelezaji wa mpango huo wa Muamala wa Karne ulio na madhara makubwa kwa taifa la Palestina na kwa maslahi ya utawala ghasibu wa Israel. Himaya inayotolewa na Marekani kwa tawala za Saudia na Bahrain imezipelekea tawala hizo kufumbia macho suala la Palestina ambalo ni suala muhimu zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu.
Kuhusu suala hilo, Karim Emile Bitar, Mkuu wa Taasisi ya Taaluma ya Masuala ya Kisiasa ya Chuo Kikuu cha St. Joseph mjini Beirut Lebanon ameashiria upinzani mkali wa wananchi wa Palestina dhidi ya mpango wa Muamala wa Karne na kusema: Kwa hakika utambulisho halisi wa mpango wa Muamala wa Karne, ni kufanyika juhudi za kuanzisha uhusiano wa kawaida na wa karibu kati ya Israel na nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi kwa gharama ya kukanyagwa haki za wananchi madhlumu wa Palestina.
Juhudi hizo ziafanyika katika hali ambayo maandamano ya mwaka huu ya Siku ya Kimataifa ya Quds, yalikuwa maonyesha makubwa ya upinzani wa mataifa ya Kiislamu na Kiarabu pamoja na makundi ya Palestina dhidi ya mpango huo wa Muamala wa Karne. Maandamano hayo mwaka huu yalifanyika katika zaidi ya nchi 100 za dunia na yalithibitisha kwamba haki na malengo matukufu ya Palestina hayawezi kubadilishwa na mpango mwingine wowote na kwamba ni 'mapambano' tu ndiyo yatakayofelisha na kuzuia utekelezaji wa mpango huo hatari wa Muamala wa Karne ambao unatekelezwa na Marekani, tawala vibaraka za Kiarabu na utawala haramu wa Israel. Carlos Santa Maria, mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa nchini Colombia anasema: Kufanyika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds kuna umuhimu mkubwa sana katika kubakisha hai suala la Palestina na tangazo la kufungamana na watu wa Palestina linapasa kuendelea kubakia hai na kudumishwa daima.
Maandamano ya mwaka huu ya Siku ya Kimataifa ya Quds, yamethibitisha kwamba hakuna kundi lolote la Palestina wala umma wa Kiislamu na Kiarabu unaounga mkono mpango wa Muamala wa Karne uliopangwa na Wamagharibi kwa ushirikiano wa baadhi ya tawala vibaraka za Kiarabu. Mpngo huo unakanyaga moja kwa moja haki za msingi za watu wa Palestina na hasa wakimbizi wa Kipalestina, na lengo lake kuu ni kudhamini maslahi ya kujipanua utawala ghasibu wa Israel katika ardhi za Waislamu na Waarabu.
Ni wazi kuwa, umoja na mshikamano wa nchi za Kiislamu utafelisha mpango huo wa Muamala wa Karne kama ilivyothibiti katika mipango mingine kama huo huko nyuma kuhusiana na suala la Palestina. Katika mazingira hayo, ni wazi kuwa tawala za kibaraka za Saudia na Bahrain kwa kuamua kutekeleza mpango huo kwa ushirikiano wa karibu wa Marekani na utawala haramu wa Israel, zinatembea kwenye kinamasi ambacho hatimaye kitawameza na kubakisha hai suala la Palestina na Quds Tukufu, ambalo linapewa msukumo na 'fikra ya mapambano.'
/129